Nigeria imedai kiti cha kudumu kwa nchi za Afrika kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kutaka kufutwa kwa deni lake linalodaiwa na wakopeshaji wa kimataifa.
Kwa sasa, Baraza la Usalama lina wanachama watano wa kudumu: Marekani, Uingereza, Ufaransa, Urusi na China.
Wote wana kura ya turufu katika azimio lolote la Baraza la Usalama.
Akihutubia mkutano mkuu wa 79 wa Umoja wa Mataifa mjini New York siku ya Jumanne, Kashim Shettima, makamu wa rais wa taifa hilo lenye watu wengi zaidi barani Afrika, alisisitiza kuwa "Baraza la Usalama linapaswa kupanuliwa."
"Bara letu linastahili nafasi katika kundi la wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama," alisema Shettima, akimwakilisha mkuu wa nchi Bola Tinubu.
'Haki na wajibu sawa'
Hiyo inapaswa kuja "na haki na wajibu sawa na wanachama wengine wa kudumu", aliongeza - hasa nguvu ya kura ya turufu.
Akizungumza na shirika la utangazaji la Marekani MSNBC, Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria Yusuf Tuggar alisema "Nigeria inahitaji kuwa katika Baraza hilo la Usalama kama mwanachama wa kudumu."
Aidha Afrika Kusini pia inakodolea macho nafsi hio.
Mapema mwezi huo, Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Linda Thomas-Greenfield, alisema Washington itaunga mkono kuundwa kwa viti viwili vya ziada vya kudumu kwa nchi za Kiafrika kwenye Baraza la Usalama.
Hata hivyo, alisema washiriki wapya hawatakuwa na haki ya kura ya turufu.
Marekebisho ya mfumo wa fedha wa kimataifa
Makamu wa rais wa Nigeria pia alitoa wito wa "mageuzi ya mfumo wa fedha wa kimataifa", akihimiza kufutwa kwa deni ambalo Nigeria inadaiwa na taasisi za kimataifa.
Shettima alisema "utaifa" na maslahi binafsi vinadhoofisha mapambano dhidi ya masuala mbalimbali ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na ugaidi, migogoro ya silaha, ukosefu wa usawa, umaskini, ubaguzi wa rangi, madeni, njaa na mabadiliko ya hali ya hewa.
Alizitaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kujitolea tena kwa ushirikiano wa pande nyingi "kudumisha umuhimu na ustahimilivu wa chombo hicho cha kimataifa."
Mapinduzi
Shettima pia alishutumu mabadiliko yasiyo ya kikatiba ya serikali katika baadhi ya nchi za Afrika katika miaka ya hivi karibuni - akimaanisha mapinduzi ambayo yamezikumba nchi nyingine za Afrika Magharibi.
Wanajeshi nchini Niger, Mali, na Burkina Faso waliingia madarakani kupitia mfululizo wa mapinduzi katika miaka ya hivi karibuni na wamejiondoa katika umoja wa kikanda wa ECOWAS.
Shettima alionya demokrasia ni "dhaifi" ikiwa haitaungwa mkono na amani, usalama, na maendeleo ya kiuchumi.