Nigeria: Mamilioni ya wasichana wapata chanjo dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi

Nigeria: Mamilioni ya wasichana wapata chanjo dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi

Maofisa wa nchi hiyo wamepongeza hatua dhidi ya virusi vinavyosababisha magonjwa ya zinaa (HPV).
Virusi vinavyosababisha magonjwa ya zinaa ndio chanzo kikuu cha saratani ya shingo ya kizazi./Picha: Unicef

Nigeria imetoa chanjo dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi kwa wasichana milioni saba nchini humo, ugonjwa unaowaathiri wasichana wadogo nchini humo.

Kampeni hiyo ya wiki mbili ni hatua kubwa katika kuwalinda wasichana wadogo na wanawake dhidi ya ugonjwa huo wenye kutishia uhai wa binadamu, kulingana na mpango wa shirika la Gavi likishirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) na Shirika la Afya Duniani (WHO).

"Ni mafanikio makubwa katika afya ya wasichana nchini Nigeria. Katika wiki mbili tu, wasichana milioni 7 wamechanjwa dhidi ya virusi vya HPV ," alisema Sania Nishtar, Afisa Mtendaji Mkuu wa Gavi.

HPV huambukizwa kwa njia ya kujamiiana na huweza kusababisha saratani ya shingo ya kizazi.

Oktoba mwaka 2023, Nigeria ilitambulisha awamu ya kwanza ya chanjo dhidi ya virusi vinavyosababisha magonjwa ya zinaa kama hatua ya kukabiliana na maradhi hayo, ambayo yanashika nafasi ya pili kati ya kansa zote zinazowakumbuka wanawake.

Waziri wa Afya wa Nigeria Muhammad Ali Pate alisema kuwa chanjo hiyo inawalenga wasichana wenye umri kati ya miaka 9 hadi 14.

Shirika la Afya Duniani linaelezea saratani ya shingo ya kizazi kama kansa ya pili yenye kuua wanawake nchini Nigeria.

Pata habari zaidi kupitia whatsapp channels

TRT Afrika