Jeshi la Nigeria limesema kuwa vikosi vyake vimewaua wapiganaji 58 haramu na kuwakamata wengine 161 katika makabiliano ya wiki mbili zilizopita Kaskazini Mashariki na Kaskazini Magharibi mwa nchi.
Msemaji wa jeshi Musa Danmadami amesema Alhamisi kuwa watu wapatao 66 waliokuwa wametekwa nyara waliokolewa huku ikipatikana pia idadi kubwa ya silaha.
Operesheni hiyo ilifanywa katika maficho ya wanamgambo wa Boko Haram na wapiganaji wanaojiita Islamic State Afrika Magharibi (ISWAP). Mamia ya jamaa na watoto waliokuwa wakiishi na wapiganaji hao waliokolewa, ameongeza kusema bwana Musa.
Nigeria imekuwa imekumbwa na mashambulio ya muda mrefu eneo la kaskazini yaliyosababisha makumi ya maelfu ya vifo na takriban watu milioni mbili kukimbia makwao. Wapiganaji hao pia wamehusika na utekaji nyara wa watu wengi kwa ajili ya kuitisha kikombozi.
Rais mpya Bola Tinubu alifanya kikao na wakuu wa mashirika ya usalama nchini humo Alhamisi kuzungumzia changamoto ya usalama.
Taarifa za ndani zimemnukuu mshauri wa kitaifa wa usalama, Babagana Monguno, akisema kuwa wamepokea maagizo kutoka kwa rais Tinubu kuwa mashirika yote husika yashirikiane.
“Ameweka wazi kabisa, kuwa mashirika yote ya usalama lazima yaoneshe ushirikiano, ushauri wao wa kila mara na kutoa ripoti kamili zitakazofuatiliwa,’’ aliongeza kusema.
Mashambulio ya Kaskazini mwa nchi yalitumiwa sana katika kampeni za uchaguzi wa Februari, baada ya kuwa wananchi wengi walilalamika kuwa hakujafanyika juhudi za kutosha kukabiliana na tatizo hilo.