Muungano wa kimataifa wa chanjo (GAVI) umesema nchi 12 barani Afrika zitapokea dozi milioni 18 za chanjo ya malaria katika kipindi cha miaka miwili ijayo.
Hii itaongeza upatikanaji wa chanjo hiyo hadi nchi tisa mpya katika kanda ya Afrika.
Nchi tisa mpya zinazotarajiwa kupokea chanjo hiyo, iliyotengenezwa na Kampuni ya dawa ya Uingereza GSK, ni Benin, Burkina Faso, Burundi, Cameroon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Liberia, Niger, Sierra Leone na Uganda.
Malaria inasalia kuwa moja ya magonjwa hatari zaidi barani, na kuua karibu watoto nusu milioni kila mwaka chini ya umri wa miaka mitano.
Mwaka 2021, Afrika ilichangia takriban 95% ya visa vya malaria duniani na 96% ya vifo, kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Chanjo ya pili
"Takriban mataifa 28 ya Afrika yameonyesha nia ya kupokea chanjo ya RTSS (malaria)," Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema katika mkutano na wanahabari Jumatano.
Ameongezea kuwa chanjo ya pili ya malaria inakaguliwa.
Ghana, Kenya na Malawi zimekuwa zikipokea chanjo ya RTS,S tangu 2019 kama sehemu ya mpango wa majaribio unaofadhiliwa na GAVI na zaidi ya watoto milioni 1.7 katika nchi hizo wamepewa chanjo hiyo, Mashirika ya GAVI, UNICEF na WHO ilisema katika taarifa ya pamoja.
Dozi za kwanza za chanjo ya RTS,S zinatarajiwa kufikia nchi 12 za Afrika katika robo ya mwisho ya 2023, na kuziruhusu kuanza kutolewa mapema mwaka ujao.