Mto Congo ni mojawapo ya vyanzo vikuu vya maji barani Afrika / Picha: AFP

Coletta Wanjohi

TRT Afrika, Istanbul

Maji yanaweza kuleta amani au kuzua migogoro. Kunaweza kuibuka misuguano na migongano katika jamii au nchi moja na nchi nyingine, iwapo rasilimali hii itaathirika au kutokupatikana kwa urahisi.

Umoja wa Mataifa unasema kuwa zaidi ya watu bilioni 3 duniani wanategemea maji yanayovuka mipaka ya nchi. Hata hivyo, ni nchi 24 pekee zilizo na makubaliano ya ushirikiano kwa maji yao yote ya pamoja.

Kadiri athari za mabadiliko ya hali ya hewa na idadi ya watu inavyoongezeka, ndivyo haja na umuhimu wa kuungana katika kulinda na kuhifadhi rasilimali yetu ya thamani zaidi inavyoongezeka.

Afya ya umma na ustawi, mifumo ya chakula na nishati, tija ya kiuchumi na uadilifu wa mazingira vyote vinategemea mzunguko wa maji unaofanya kazi vizuri na unaosimamiwa kwa usawa.

Mizozo ya maji Afrika

Barani Afrika kumekuwa na mivutano kadhaa kuhusu rasilimali hii.

Kwa mfano Misri , Ethiopia na Sudan zinazozana kuhusu maji ya Mto Nile .

Kwa upande mwingine, Misiri na Sudan zinavutana na Ethiopia kuhusu ujazaji na uendeshaji wa kila mwaka wa Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance (GERD).

Bwawa la GERD linajengwa na Ethiopia na linatarajiwa kuwa na uwezo wa kuzalisha Megawati 6000 za umeme.

Bwawa la GERD nchini Ethiopia./Picha:TRT Afrika

Misri inadai kuwa itaathiri mtiririko wa maji kuelekea kwake, hoja inayoungwa mkono na Sudan.

Lakini Ethiopia imesema inahitaji bwawa hili kwa ajili ya kufua umeme kwa wananchi wake na kuwakwamua kutoka kwenye umasikini.

Mwaka huu mzozo mpya umezuka kati ya Ethiopia na Somalia kuhusu bandari.

Makubaliano yaliyotiwa saini mjini Addis Ababa kati ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed na Rais wa wa eneo lililojitenga la Somaliland Muse Bihi Abdi, yataifungulia Ethiopia njia kuanzisha shughuli za kibiashara za baharini na kuipa ufikiaji wa kituo cha kijeshi kilichokodishwa kwenye Bahari Nyekundu.

Somalia imepinga hoja hii, ikidai kuwa eneo la Somaliland ni sehemu ya Somalia na haina mamlaka ya kutoa sehemu ya bahari na bandari.

Ziwa Victoria kama kiunganishi

Hata hivyo kuna maji mengine ambayo yameleta umoja.

Ziwa Victoria ni mojawapo ya Maziwa Makuu ya Afrika. Likiwa kilomita za mraba 59,947, Victoria ndio Ziwa kubwa zaidi barani Afrika kwa eneo na ziwa kubwa zaidi la kitropiki duniani, likipatikana Tanzania, Kenya na Uganda.

Nchi hizi zimeweka mamlaka ya pamoja ya kuhakikisha kuwa ziwa hilo linawahudumia wanachi wa nchi zote tatu bila kuhitalifiana.

Ziwa hilo limeajiri takriban watu 200,000 katika uvuvi wa moja kwa moja na kusaidia maisha ya watu milioni nne. Wataalmu wanasema ziwa hilo linazalisha zaidi ya dola milioni 150 katika mapato ya mauzo ya nje, na ni chanzo cha lishe bora kupitia protini ya samaki yenye ubora wa juu kwa takriban watu milioni nane katika bonde hilo.

Mbali na kuvua samaki maji ya Ziwa Victoria hutumika pia katika michezo mbali mbali/ Picha/:Reuters 

Ziwa ni njia muhimu ya usafiri inayounganisha Mataifa ya Afrika Mashariki, ni hifadhi ya vituo vinne vya kuzalisha umeme wa maji kando ya Mto Nile, huku ikitoa maji kwa matumizi ya viwandani na nyumbani, na kudhibiti hali ya hewa ya ndani.

Ina idadi kubwa zaidi ya maeneo ya mijini katika bonde lake la Maziwa Makuu yote ya Afrika, na maeneo oevu yake hupokea na kutibu maji machafu kutoka maeneo ya mijini na ya kilimo.

Hata hivyo, Ziwa hilo linakabiliwa na changamoto za ukataji miti, mabadiliko ya matumizi ya ardhi, uharibifu wa ardhi oevu na kumwaga maji kutoka maeneo ya mijini, viwanda na mashamba.

TRT Afrika