Ishmael Chokurongerwa hakuwa tayari kuzungumza na vyombo vya habari./ Picha:Reuters  

Kiongozi wa kikundi cha dini nchini Zimbabwe amekosa dhamana, wiki moja baada ya kukamatwa kwa tuhuma za kunyanyasa watoto 251 kwa kuwatumikisha shambani mwake.

Ishmael Chokurongerwa, mwenye miaka 56, ambaye pia anajiita nabii, alifikishwa mahakamani katika mji wa Norton ulio karibu na mji mkuu wa Harare siku ya Jumanne, akiwa ameambatana na viongozi wengine saba wa kanisa hilo. Watuhumiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote baada ya kufikishwa mahakamani hapo.

Akiwanyima watuhumiwa hao dhamana, Hakimu Mkazi wa Norton Christine Nyandoro alidai kuwa Chokurongerwa alitumia ushawishi wake kwa mashahidi, na maamuzi ya kuwaachia kwa dhamana yataibua mjadala nchini humo.

Makaburi yasiyosajaliwa

Watuhumiwa hao wamepatikana na makosa ya ukiukwaji wa sheria ya Maziko na ile ya Watoto, baada ya polisi kukuta watoto 251 wakitumikishwa na kufanyishwa kazi ngumu katika mashamba na makaburi.

Watuhumiwa hao watabaki rumande kuanzia Aprili 4, wakati wa kusikilizwa kwa shauri hilo.

Chokurongerwa, ambaye pia anafahamika kama Madzibaba Ishmael, alitambulika na polisi wa Zimbabwe kama kiongozi wa kanisa la Johane Masowe au "vazi jeupe", ambapo waumini wake wanatuhumiwa kunyanyasa watoto nchini Zimbabwe.

Kugoma kuzungumza

Wakiwa wamevalia mavazi meupe, wengi wa wafuasi hao walifika kusikiliza shauri hilo mahakamani siku ya Jumanne lakini waligoma kuzungumza na waandishi wa habari. Chokurongerwa, ambaye alifunika kichwa chake kwa taulo, pia hakuwa tayari kuzungumza.

Mwanasheria wa watuhumiwa hao, Purity Chikangaise, aliweka wazi nia ya kukata rufaa ili wapate dhamana kutoka Mahakama Kuu.

"Tutakata rufaa maamuzi ya mahakama hii," alisema.

TRT Afrika