Umoja wa Afrika AU, umeelezea "wasiwasi mkubwa" juu ya mlipuko wa vita wa hivi karibuni wa vurugu kati ya Israeli na Palestina ukisema kuwa una "matokeo mabaya" kwa maisha ya raia na amani ya kikanda.
"Kukataliwa kwa haki za kimsingi za Watu wa Palestina, haswa ile ya serikali huru, ndio sababu kuu ya mvutano wa kudumu kati ya Israeli na Palestina," mwenyekiti wa AU Moussa Faki Mahamat alisema kupitia taarifa.
Wakati huo huo, Faki alitoa wito kwa pande zote mbili "kukomesha uhasama wa kijeshi haraka na kurudi, bila masharti, kwenye meza ya mazungumzo kutekeleza mpango wa kuunda nchi mbili zitakazoishi bega kwa bega.''
Moussa Faki Mahamat anaamini hii " italinda maslahi ya watu wa Palestina na watu wa Israel.''
Hamas ilitekeleza shambulio la kushangaza Jumamosi ambalo lilishirikisha wapiganaji kadhaa walioingia katika miji ya Israeli karibu na ukanda wa Gaza huku kukiwa na moto mkali wa roketi na vurugu zilizokuwa zikiendelea hadi kuingia jumapili.
Angalau Waisraeli 300 waliuawa na zaidi ya 1,500 walijeruhiwa katika shambulio hilo, wakati askari kadhaa na raia walikamatwa na Hamas na kupelekwa Gaza.
Aidha, Israel ililipiza kisasi baadaye kwa mfululizo wa mashambulizi ya anga haswa katika ukanda wa Gaza, ambayo yaliwauwa zaidi ya Wapalestina 250 na kuwajeruhi zaidi ya 1,700, kulingana na Wizara ya Afya ya Palestina.
Ukumbusho wa vita vya 1973
Kufuatia kuzuka kwa vurugu, Waziri mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu aliapa kutumia nguvu zote za Israeli kuharibu uwezo wa Hamas na "kulipiza kisasi kwa siku hii nyeusi.”
Wizara ya mambo ya nje ya Iran ilielezea shambulio la Hamas kama kitendo cha kujitetea. Iran ni adui mkubwa wa Israel.
Shambulio la Hamas lilijiri wakati Israeli iliadhimisha miaka 50 ya vita vya 1973 ambavyo vilipelekea Tel Aviv karibu na kushindwa kwa idadi kubwa ya maafa.