Mzozo wa DRC na Rwanda tayari umeleta hofu katika eneo na hata nje ya Afrika.
Sio jambo geni kwamba Mashariki mwa DRC imekumbwa na migogoro ya ndani na wakati mwingine imehusisha nguvu za nje.
Habari za punde zaidi kutoka huko ni kuwa Majeshi ya Congo yamejiondoa kutoka mji wa Bukavu na viunga vyake, hii ni baada muungano wa waasi ukiongozwa na M23 kuendelea kuteka vijiji na miji. Wameteka Goma, Bukavu ikiwemo uwanja wa ndege na maeneo mengine muhimu.
Majeshi ya Burundi ambayo yamekuwa Mashariki mwa Congo tangu 2022 yamejiondoa.
Haijulikani kwa uhakika idadi kamili ya wanajeshi wa Burundi ndani ya DRC. Hata hivyo Burundi ina mpaka wa kilomita 243 na DRC. Sehemu kubwa yake inapitia mto Rusizi/Ruzizi upande wa kaskazini na Ziwa Tanganyika upande wa kusini. Imeelezwa kuwa mojawapo ya mipaka inayoweza kupenyeka kirahisi zaidi katika eneo la Maziwa Makuu barani Afrika.
Kwa upande mwingine Malawi pia ilikuwa na wanajeshi wake ndani ya DRC lakini mwanzoni mwa mwezi Februari, Rais wa Malawi aliagiza majeshi yake kuondoka humo.
Majeshi ya Malawi yalikuwa kati ya kikosi cha SADC ambapo kwa sasa waliobakia katika kikosi hiki ni majeshi ya Afrika Kusini na yale ya Tanzania.
Uganda nayo, ambayo tayari ilikuwa na majeshi yake kadhaa ndani ya mpaka ya DRC kwa sababu za kulinda mipaka yake dhidi ya waasi wa ADF, imetangaza kupeleka wanajeshi zaidi katika eneo la Bunia, ambako inasema itasaidia Watutsi wanaoshambuliwa huko
Lakini huku M23 wakionekana kuendelea kuteka maeneo zaidi mashariki mwa DRC, ghadhabu zinazuka nje ya eneo hilo na hata kutoka mataifa ya magharibi.
Rwanda imejikuta ikilaumiwa kwa kudaiwa kufadhili waasi wa M23, jambo ambalo Rwanda imekanusha.
Licha ya hayo, shutma za kimataifa zimeendelea kuelekezewa Rwanda.
Wiki hii Uingereza imemtaka Balozi wa Rwanda kutoa maelezo kuhusu madai yanayoihusisha na M23.
Na Rwanda pia imeghadhabishwa na hatua ya Ubelgiji kuegemea upande wa DRC katika mzozo huu, na hivyo imesitisha uhusiano wake wa kibiashara na Ubelgiji.
Nchi za Magharibi zimekemea mzozo unaoendelea lakini zinaonekana imma hazina uwezo kutatua mgogoro huu au zinasuwasuwa kutokana na maslahi.
Mataifa hayo yana makampuni yao mengi ndani ya DRC yanayochimba madini.
Mzozo wa DRC, unasemekana kuwa wa Kikabila, kuhusisha Watutsi wa Mashariki mwa Congo ambao Rwanda na Uganda wanadai kuwalinda. Au ni rasli mali zake, ambazo mataifa mingi hasa ya magharibi yanayatolea macho. Unadhani nani anafaidi zaidi katika mgogoro huu usiokwisha?