Mwaka 2025 unavyoingia, ndivyo mgogoro wa Sudan katika pembe ya Afrika, unavyoingia hatua nyengine.
"Kijiji chetu kilikuwa kinawaka moto," anasema Alhida Hammed, ambaye sasa anatibiwa jeraha la risasi katika Hospitali ya Kaunti ya Renk, nchini Sudan Kusini.
Hammed na maelfu wengine walikimbia jimbo la Blue Nile nchini Sudan huku sehemu za nchi yake ikikumbwa na mapigano tangu Aprili 2023, kati ya Vikosi vya Wanajeshi wa Sudan na Kikosi cha Msaada wa Haraka, RSF.
“Nyumba zilikuwa zinawaka moto, na kila mtu alikuwa akikimbia upande tofauti. Tumehamishwa na sasa tunaishi chini ya mti. Sina hamu ya kurudi nyumbani. Nyumbani si nyumbani tena—kumejaa kumbukumbu mbaya,” Hammed anasema.
Anatibiwa na Médecins Sans Frontières (MSF) pia inajulikana kama Madaktari Wasio na Mipaka, ambao inasema kuwa zaidi ya watu 5,000 wamevuka hadi Sudan Kusini kila siku tangu mwanzoni mwa Disemba 2024, huku wakitoroka mapigano nchini Sudan.
Mapigano yanayoendelea karibu na mpaka katika majimbo ya White Nile ya Sudan, Blue Nile na Sennar yamewalazimu watu kuingia katika mji wa Renk nchini Sudan Kusini.
"Tumeongeza mahema 14 kuzunguka hospitali ili kutoa nafasi kwa wagonjwa waliojeruhiwa na vita ambao wanawasili katika Hospitali ya Kaunti ya Renk," anasema Emanuele Montobbio, Mratibu wa dharura wa MSF huko Renk.
"Hakuna mahali pa mahema mengine katika mazingira, wakati wagonjwa na familia zao wanaendelea kuja hospitali."
UNHCR inakadiria kuwa hadi tarehe 22 Disemba 2024 idadi ya waliohamishwa kutoka Sudan ilikuwa 12,250,024.
Kati ya hao waliotafuta hifadhi nje ya nchi ni 3,206,189.
Mzozo huo umegharimu maisha watu zaidi ya 29,000 kulingana na UN.
Chad, Libya, Misri, Ethiopia, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Sudan Kusini zinapokea wakimbizi kutoka Sudan.
Kufikia tarehe 23 Disemba 2024, madakitari wa MSF wanasema wamepokea zaidi ya wahamiaji wapya 80,000 kutoka Sudan wanaovuka kuingia Sudan Kusini ambao walikuwa wakihitaji matibabu.
Ni watu wachache tu wameripotiwa kutibiwa kwa upasuaji na chanjo ya pepopunda katika wiki za hivi karibuni, huku zaidi ya wagonjwa 100 waliojeruhiwa, wengi wao wakiwa na majeraha mabaya, bado wanasubiri upasuaji.
Ukosefu wa chakula
Kwa wale ambao wamesalia nchini Sudan, njaa inaongeza ukosefu wa usalama.
27 Disemba 2024, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP limesema watu 78,000 Kusini mwa mji mkuu Khartoum walipokea msaada wa chakula na lishe kwa mara ya kwanza tangu mzozo huo uanze Aprili 2023.
Mapigano hayajaruhusu kufikiwa kwa msaada huo kwa zaidi ya miezi 20.
Ripoti ya hivi majuzi ya Umoja wa Mataifa inaonya kwamba zaidi ya watu milioni 24.6 kote nchini Sudan, ambao ni zaidi ya nusu ya idadi ya watu wanakabiliwa na viwango vya juu vya uhaba wa chakula.
Kati ya hawa milioni 8.1 wako katika hali za dharura huku zaidi ya 638,000 wakiwa katika kile kinachojulikana kama hatua ya janga.
"Shirika la Chakula na Kilimo, FAO lina wasiwasi mkubwa juu ya hali mbaya ya usalama wa chakula nchini Sudan, haswa katika kambi ya wakimbizi ya ndani ya Zamzam na makazi mengine katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro, ambapo hali inazidi kuwa mbaya, na watu wengi zaidi wanaingia katika hali ya dharura au njaa,” alisema Mkurugenzi wa Dharura na Ustahimilivu wa FAO, Rein Paulsen.
Wakati 2024 inaisha Sudan imekosa msimu wa mavuno, wakati upatikanaji wa chakula unapaswa kuwa wa juu zaidi.
"Njaa ya muda mrefu imetanda nchini Sudan," amesema Mkurugenzi wa Uchambuzi wa Usalama wa Chakula na Lishe wa WFP, Jean-Martin Bauer.
"Watu wanazidi kudhoofika na wanakufa kwani wamekuwa na uwezo mdogo wa kupata chakula kwa miezi kadhaa," Bauer ameongezea.
Kwa kuendelea kwa mapigano Sudan inaweza kukosa msimu ujao wa kupanda pia.
"Mamilioni ya maisha ya vijana hutegemea utoaji wa chakula na matibabu ya kuokoa maisha. Pia maji na dawa inaweza kusaidia kukomesha janga la utapiamlo lakini tunahitaji ufikiaji salama, endelevu na usiozuiliwa ili kuwafikia watoto walio hatarini zaidi na kuokoa maisha," Mkurugenzi wa Operesheni za Dharura wa UNICEF, Lucia Elmi amesema.
Suluhu ni nini?
Juhudi za mwaka 2024 za kunyamazisha bunduki nchini Sudan zimegonga mwamba.
Umoja wa Afrika umesisitiza kuwa wadau wa Sudan lazima watafute suluhu ya ndani ya tatizo hilo.
Lakini juhudi za shirika la kikanda la Jumuiya ya Kiserikali ya Maendeleo IGAD, pamoja na jirani ya Sudan Kusini mwa Sudan, hazijazaa matokeo yanayotarajiwa, mapigano yameendelea.
Uturuki sasa inajitolea kuunga mkono jitihada za amani nchini Sudan kwa upatanishi kati ya Sudan na Umoja wa Falme za Kiarabu, UAE.
Kuhusika kwa UAE, hasa kwa kuchochewa na maslahi ya kimkakati kama vile kupata njia za meli za Bahari Nyekundu na uwekezaji katika maliasili ya Sudan, kumeongeza ugumu katika mgogoro nchini Sudan.
Wakati Sudan inathamini michango ya kiuchumi ya UAE, sera za Abu Dhabi zimezua maswali kuhusu ushawishi wa nje katika masuala ya ndani ya Sudan.
"Tunatumai kwamba mipango iliyowekwa, ikiwa ni pamoja na pendekezo la kiongozi mwenye busara na uzoefu Erdogan, ambaye alionyesha utayari wake wa kupatanisha Sudan na UAE baada ya upatanishi uliofanikiwa kati ya Ethiopia na Somalia," Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan Ali Youssef alisema.
Waziri wa Sudan alisema kuwa RSF ilikataa kufuata masharti ya "makubaliano ya Jeddah" yaliyotiwa saini Mei 2023.
Hadi suluhu ipatikane, maisha ya watu Sudan yamejawa na kukata tamaa, huku jukumu ya kurejesha amani ikiwa mikononi mwa majenerali wawili, wanaoongoza Jeshi la Sudan na kikosi cha Rapid Support Focres, RSF.