Mahakama katika mji mkuu Kinshasa siku ya Jumatatu ilimpata Bujakera na hatia ya kueneza habari za uongo miongoni mwa mashtaka mengine./ Picha wengine 

Stanis Bujakera, mwandishi wa habari aliyezuiliwa tangu Septemba mwaka jana katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa tuhuma za kueneza habari za uongo, aliachiliwa Jumanne, wakili wake alisema.

Wakili, Yana Ndikulu, alisema Bujakera - ambaye anafanya kazi katika vyombo vya habari vya kimataifa ikiwa ni pamoja na Reuters na Jeune Afrique - aliachiliwa Jumanne jioni kutoka jela katika mji mkuu Kinshasa alikokuwa akishikiliwa.

“Mteja wetu yuko huru,” Ndikulu alisema.

Bujakera aliiambia Reuters mkurugenzi wa gereza alimwambia kuwa yuko huru kuondoka muda mfupi baada ya saa tatu usiku saa za ndani (2030GMT).

Mahakama katika mji mkuu Kinshasa siku ya Jumatatu ilimpata Bujakera na hatia ya kueneza habari za uongo miongoni mwa mashtaka mengine.

Ilimhukumu kifungo cha miezi sita jela na kumpiga faini ya faranga za Kongo milioni 1 ($364). Timu yake ya wanasheria ilisema baada ya uamuzi huo kwamba Bujakera ataachiliwa Jumanne kwa sababu tayari alikuwa ametumikia kifungo chake.

Lakini kuachiliwa huru kulisitishwa bila kutarajiwa baada ya habari kuibuka Jumanne jioni kwamba mwendesha mashtaka wa serikali katika kesi hiyo alikuwa amekata rufaa dhidi ya hukumu hiyo. Takriban saa tatu baadaye hata hivyo, mawakili wa Bujakera walisema mwendesha mashtaka alikuwa ameondoa rufaa yake, na hivyo kuandaa njia ya kuachiliwa kwake.

"Kutokana na kile tunachoelewa, mwendesha mashtaka hatimaye aliondoa rufaa, ambayo iliruhusu kuachiliwa kwa kuchelewa," Ndikulu aliiambia Reuters.

Bujakera alikamatwa mwezi Septemba kwa tuhuma za kueneza habari za uongo kuhusu mauaji ya mwanasiasa mashuhuri wa upinzani katika makala iliyochapishwa na Jeune Afrique, gazeti la habari la Ufaransa limesema.

Mwendesha mashtaka katika kesi hiyo mapema mwezi huu alikuwa ameitaka mahakama ya Kinshasa kumhukumu Bujakera kifungo cha miaka 20 jela.

Mashirika ya haki za ndani na kimataifa yakiwemo Reporters Without Borders na Amnesty International yalilaani kuzuiliwa kwa Bujakera, na kuiita shambulio dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari. Reuters pia imetoa wito wa kuachiliwa kwake.

Reuters