Serikali ya Rwanda ilimshutumu rais wa Burundi kwa kuchochea migawanyiko kati ya Wanyarwanda huku kukiwa na uhusiano mgumu.
Hatua hiyo ilifuatia ripoti za Jumapili zilizoonyesha kwamba alipokuwa akiwahutubia vijana katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, rais Evariste Ndayishimiye alisema Wanyarwanda walihitaji "kuanza kuweka shinikizo" kwa viongozi wao kwa sababu "ninaamini kuwa vijana wa Rwanda hawawezi kukubali kuwa wafungwa katika eneo hilo."
Ndayishimiye aliripotiwa kuwahutubia vijana katika nafasi yake ya Bingwa wa Umoja wa Afrika kwa Vijana, Amani na Usalama.
Katika taarifa yake siku ya Jumatatu, serikali ya Rwanda ilichukizwa na kile ilichokiita kauli za uchochezi na zisizo za Kiafrika.
Kuhatarisha amani
Rwanda Ilimshutumu kiongozi huyo wa Burundi kwa "kuchochea migawanyiko kati ya Wanyarwanda na kuhatarisha amani na usalama katika eneo la maziwa makuu."
“Wanyarwanda wamefanya kazi kwa bidii ili kuimarisha umoja na maendeleo ya nchi. Vijana wa Rwanda wamechangamkia fursa hii na wanachukua umiliki na kuchangia katika kujijengea maisha mema,” ilisema taarifa ya ofisi ya msemaji wa serikali.
"Kwa mtu yeyote kujaribu kudhoofisha maendeleo haya kwa kutoa wito kwa Wanyarwanda kupindua serikali yao inatia wasiwasi. Lakini kiongozi wa nchi jirani kufanya hivyo, kutoka jukwaa la Umoja wa Afrika, ni kutowajibika sana na ni ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Umoja wa Afrika, ” iliongeza.
Ripoti hiyo ilizua taharuki kwenye mitandao ya kijamii miongoni mwa Wanyarwanda.
Uhusiano wa mvutano
Lakini balozi wa Burundi katika Umoja wa Afrika Willy Nyamitwe, alisema ripoti zinazohusishwa na Ndayishimiye hazikuwa sahihi.
Shutuma hizo zinakuja huku kukiwa na uhusiano ambao tayari umeyumba baada ya Burundi kufunga mpaka wake na Rwanda mapema mwezi huu kufuatia shutuma kwamba jirani yake inaunga mkono waasi wa Burundi walioko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, madai ambayo Rwanda inakanusha.
Rwanda ilisisitiza Jumatatu kwamba haina nia ya kuanzisha migogoro na majirani. "Tutaendelea kufanya kazi na washirika katika kanda na kwingineko ili kuimarisha utulivu na maendeleo endelevu," ilisema taarifa hiyo.