Marais wa Afrika wamenza kuelekea Urusi kwa mkutano wa Afrika na Urusi .
Mkutano huo ambao umepangwa kufanyika mjini St Petersburg siku ya Alhamisi na Ijumaa utahudhuriwa na Rais Vladmir Putin ambaye anatarajiwa kufanya mazungumzo ya kina ya moja kwa moja na viongozi binafsi wa Afrika,
Ikulu ya Uganda imetangaza kuwa Rais Yoweri Museveni ameeleka Urusi.
" Leo asubuhi, Rais Yoweri Kaguta Museveni aliondoka kuelekea Urusi kuungana na viongozi wengine wa Afrika kwa ajili ya Kongamano la pili la Uchumi na Kibinadamu la Urusi-Afrika linalopangwa kufanyika tarehe 27-28 Julai mjini Saint Petersburg." ikulu imesema katika mtandao wa X ( twitter).
Eritrea pia imetangaza safari ya rais Isaiyas Aferwerki.
"Kwa mwaliko wa Rais Vladmir Putin, Rais Isaias Afwerki ameondoka leo asubuhi kuelekea Urusi kushiriki Mkutano wa Russia-Africa Summit utakaofanyika St. Petersburg kuanzia tarehe 27-28 Julai wiki hii," msemaji wa rais Yemane Meskel amesema katika Twitter.
Ofisi ya ya rais wa Burundi Évariste Ndayishimiye pia imesema rais huyo ameelekea Urusi kwa mkutano huo .
Urusi yashutumu nchi za magharibi
Ikulu ya Kremlin imezishutumu nchi za Magharibi na hasa Marekani kwa kujaribu kuhujumu mkutano wake na Afrika kwa kuzishinikiza nchi za Afrika kutoshiriki.
Mazungumzo yao inaripotiwa kuwa yatazingatia kila kitu kuanzia biashara hadi usalama, mikataba ya silaha na vifaa vya nafaka.
Katika mkutano huu mikataba mbalimbali inatarajiwa kutiwa saini. Mkutano huu unafuata mkutano wa kwanza wa marais kati ya Urusi na Afrika mwaka 2019.
''Wajumbe 49 wa Afrika wamethibitisha ushiriki wao, karibu nusu yao wakiwakilishwa na wakuu wao wa nchi au serikali,'' mwanadiplomasia wa Urusi Alexander Polyakov alinukuliwa akisema na shirika la habari la TASS mapema mwezi huu.
Lakini msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alisema Jumanne kwamba nchi za Magharibi zinafanya kila juhudi kuharibu mkutano huo na Urusi.
"Takriban mataifa yote ya Kiafrika yamekuwa chini ya shinikizo kubwa kutoka kwa Marekani, na balozi za Ufaransa chini mwao pamoja na wajumbe wengine wa Magharibi ambao pia wanajaribu kufanya jitihada zao ili kuzuia mkutano huu usifanyike," Peskov aliiambia waandishi wa habari.
"Kimsingi, hawakubali haki ya uhuru ya mataifa ya Afrika ya kuamua kwa uhuru washirika wao kwa ushirikiano na mwingiliano wa pande zote katika nyanja mbalimbali."
Rais wa Marekani Joe Biden aliandaa mkutano wa marais wa viongozi wa Afrika na Marekani mjini Washington mwaka jana, akitaka kuimarisha ushirikiano huku kukiwa na ongezeko la uwepo wa Urusi na China katika bara hilo.