Vita vinavyoendelea Sudan vimetatiza usambazaji wa chakula. /Picha: AFP

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres Jumanne ameelezea wasiwasi wake kuhusu kuongezeka kwa ukosefu wa chakula nchini Sudan, akionya juu ya hali ya njaa katika maeneo kadhaa huku mzozo ukiendelea.

"Katibu Mkuu amesikitishwa na hali inayozidi kuwa mbaya ya usalama wa chakula nchini Sudan, huku upatikanaji wa chakula na lishe kwa mamilioni ya watu nchini kote ukiendelea kuzorota kulingana na ripoti iliyotuliwa na Kamati ya Uanishaji wa Hatua za Usalama wa Chakula (IPC)," msemaji Stephanie Tremblay amesema katika taarifa.

Ikisema kwamba "ripoti ya hivi punde ya Kamati ya IPC inaonyesha kuwa hali ya njaa iko katika angalau maeneo matano nchini Sudan," taarifa hiyo imeonyesha kambi za watu waliokimbia makazi yao huko Darfur Kaskazini na Milima ya Nuba magharibi huko Kordofan Kusini kama maeneo yenye hatari.

Zaidi ya hayo, maeneo mengine matano yanaonekana kuwa katika hatari ya njaa katika miezi ijayo, kulingana na IPC.

Ikisisitiza kuwa "zaidi ya watu milioni 24.6 nchini Sudan, zaidi ya nusu ya idadi ya watu, wanakabiliwa na viwango vya juu vya uhaba wa chakula" kutokana na mzozo huo, taarifa hiyo ilisema zaidi kwamba "mapigano yanayoendelea na vikwazo vya usafirishaji wa misaada na wafanyikazi vinaendelea kuhatarisha shughuli za utoaji msaada."

Guterres amerudia "wito wake kwa wahusika kuwezesha ufikiaji wa haraka, salama, bila vikwazo na endelevu ili msaada wa kibinadamu na wafanyikazi waweze kuwafikia watu wanaohitaji popote walipo."

"Katibu Mkuu pia amesisitiza haja ya kusitishwa mara moja kwa uhasama ili kuokoa maisha na kuzuia mzozo wa Sudan na athari zake kuongezeka zaidi katika nchi jirani mnamo 2025," ripoti hiyo imesema, huku akiomba uungwaji mkono zaidi wa kimataifa kushughulikia mgogoro unaoongezeka na kuitaka jumuiya ya kimataifa kuongeza ufadhili kwa shughuli za kibinadamu nchini Sudan.

Tangu Aprili 2023, Sudan imekuwa ikikabiliwa na mapigano makali kati ya jeshi na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) kuhusu suala la mageuzi ya kijeshi na masuala ya ushirikiano.Mzozo huo umegharimu maisha ya zaidi watu 20,000, huku mamilioni ya watu kuyahama makazi yao na wengine zaidi ya milioni 25 wakihitaji msaada wa kibinadamu, kulingana na UN.

AA