Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameelezea wasiwasi wake juu ya kukamatwa kwa waangalizi wa uchaguzi, ripoti za vitisho vya wapiga kura pamoja na vitisho vya ghasia kufuatia uchaguzi wa Zimbabwe.
Wiki iliyopita, Zimbabwe ilifanya uchaguzi, na kuchagua rais, wabunge na madiwani.
Lakini matokeo ya uchaguzi huo yalipingwa na Chama cha Upinzani cha Citizens Coalition for Change (CCC) kilichodai kuwa tume ya uchaguzi ya Zimbabwe ilitangaza matokeo feki ya uchaguzi wa urais yaliyomtangaza Rais Emerson Mnangagwa kuwa mshindi kwa asilimia 52.6 huku Nelson Chamisa wa muungano wa wananchi wa mageuzi akipata 44%.
"Katibu mkuu anatoa wito kwa viongozi wa kisiasa na wafuasi wao kukataa aina yoyote ya unyanyasaji, vitisho vya vurugu, au uchochezi wa ghasia, na kuhakikisha kuwa haki za binadamu na sheria zinaheshimiwa kikamilifu," ilisema taarifa ya UN siku ya Jumapili.
Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alihimiza maazimio "kwa njia ya haki, ya haraka, na ya uwazi ili kuhakikisha kwamba matokeo ya (uchaguzi) ni onyesho la kweli la mapenzi ya watu."
Ukosefu wa karatasi za kupigia kura
Katika uchaguzi wa Jumatano nchini Zimbabwe, upigaji kura uliongezwa hadi Alhamisi katika baadhi ya maeneo, ikiwa ni pamoja na Harare, mji mkuu wa nchi hiyo, kutokana na ukosefu wa karatasi za kupigia kura.
Kufuatia uchaguzi ambao ulielezwa kuwa ulijaa na dosari nyingi, Mnangagwa alipata muhula wa pili wa miaka mitano baada ya kutangazwa kwa matokeo kuelekea saa sita usiku Jumamosi.
CCC ya Chamisa imekataa matokeo ya uchaguzi wa urais ikisema yalikumbwa na "udanganyifu mkubwa."
“Hatutasubiri kwa miaka mitano. Lazima kuwe na mabadiliko sasa,” Chamisa aliwaambia wanahabari Jumapili.
Wakati huo huo, waangalizi wa uchaguzi kutoka mtandao wa kusaidia uchaguzi wa Zimbabwe na kituo cha rasilimali za uchaguzi wamedai kuwa polisi walivamia vituo vyao vya data, wakidai walikuwa wakinyanyaswa ili kuwazuia kuhakiki matokeo kwa uhuru.