Na Kevin Philips Momanyi
TRT Afrika, Instanbul, Uturuki
“Sio kweli.” Mke wa zamani wa Kaka anakanusha uvumi kwamba alitalikiana na mchezaji huyo kwa sababu alikuwa ‘mkamilifu sana’.
Mke wa zamani wa mchezaji wa kimataifa wa Brazil na nyota wa zamani wa AC Milan na Real Madrid, Ricardo Kaka, Caroline Celico, amekanusha uvumi uliotapakaa kuhusu kuachana kwao.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Celico alisema “Kwa bahati mbaya tunasikia habari za uongo na nukuu FEKI. Ngoja niwaeleze ukweli. Nilitalikiana karibu miaka 10 iliyopita... hata hivyo nilipata wawili wa kupendeza ndani ya miaka hiyo 14 ya uhusiano."
Celico amesisitiza kuwa kuachana kwao kulitokana na makubaliano yao wawili, licha ya uvumi kwamba alimwacha Kaka kwa sababu alikuwa mkamilifu sana.
“Imekuwa karibu miaka 8. Niko na mume wangu Eduardo, na tutapata mtoto wetu wa kwanza mwezi ujao Ninaheshimu sana simulizi ya maisha yangu, na ninashukuru sana kwa kila kitu ambacho nimeishi hadi sasa. Mume wangu wa zamani na mimi tulipitia njia nzuri ya kulea watoto wetu, na ninashukuru sana kwa hili," aliongeza.
Kaka alifunga ndoa na Celico, mpenzi wake wa utotoni, huko São Paulo nchini Brazil mnamo 2005; kabla ya kutengana miaka 10 baadaye.
Wawili hao walijaliwa watoto wawili, Luca Celico Leite, aliyezaliwa Juni 10, 2008 na Isabella Celico Leite aliyezaliwa Aprili 23, 2011.
Kutengana kwao, kulikuwa kwa kimya hadi hivi majuzi, baada tetesi kuanza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Wakati huo huo, Kaka mwenye umri wa miaka 41, ameingia kwenye mahusiano na binti mwingine wa Kibrazil Carolina Dias toka 2016, mwaka mmoja baada ya kutalikiana na Celico.
Wawili hao wamejaliwa kupata mtoto mmoja wa kike.