Madakitari wanasema serikali haijawatimizia haki katika maslahi ya malipo / Picha: AFP

Wataalamu wa afya pamoja na wanafunzi madaktari nchini Kenya wametishia kuendelea na mgomo wao iwapo serikali haitawapa mahitaji yao.

Wataalamu hao wa afya, wanapanga kufanya maandamano ya amani siku ya Ijumaa katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.

Muungano wa Madaktari, Wafamasia na Madaktari wa Meno nchini Kenya, KPMDU, uliipa serikali notisi ya mgomo kutoka tarehe Machi 13, 2024, ikiwa serikali itashindwa kutatua changamoto zao.

Madaktari hao wanaitaka serikali kuwatuma kazini wanafunzi wahudumu wa afya mara moja na kufuta malimbikizo ya mishahara ya madaktari kulingana na Makubaliano ya Pamoja ya 2017.

"Hayo ni mambo ambayo yanafaa kutekelezwa,” Katibu Mkuu wa Muungano wa Madaktari wa Meno wa Kenya Davji Atellah alisema wiki jana.

Madaktari na wataalamu wengine wa afya wanaitaka serikali kutimiza mahitaji yao, la sivyo wataweka chini vifaa vyao vya kazi.

Wahudumu wa afya ambao wamehudumu kwa miaka minne chini ya kandarasi katika taasisi za afya ya umma wanadai ajira ya kudumu ambayo walikuwa wamehakikishiwa na serikali ya Kenya kufuatia miaka mitatu ya huduma.

Baadhi ya madaktari wakiandamana kuelekea Bunge la nchi hiyo jijini Nairobi. / Picha: AFP

Masuala muhimu yaliyoibuliwa na KMPDU ni pamoja na kucheleweshwa kwa kazi ya kuajiriwa hasa kwa madaktari wapya waliomaliza masomo yao.

Serikali imetishia kuwafuta kazi madaktari hao iwapo wataendelea na mgomo huo.

Lakini huku mgomo huo ukiingia siku ya nane Alhamisi, Waziri wa Afya Susan Nakhumicha anasisitiza kuwa madaktari hao wanakiuka agizo la mahakama linalotaka kusitisha mgomo huo na wana hatari ya kupoteza kazi zao kwa kukosa kuripoti kazini.

“Wameamriwa na mahakama kusitisha mgomo; kila kitendo kina matokeo,” Waziri wa Afya alisema Jumatano usiku katika mahojiano na moja wapo ya vyombo vya habari vya nchi hiyo.

"Ikiwa unatakiwa kuwa kazini na hauko kazini, tutapata mtu mwengine wa kufanya kazi hiyo," Nakhumicha alisema, akisisitiza kwamba wahudumu wa afya watatumwa kuanzia mwezi ujao.

Jumatano, Hospitali ya Taifa ya Kenyatta iliushtaki Muungano wa Madaktari mahakamani ikiwataka wasitishe mgomo wao ulioanza wiki jana.

Jaji Byram Ongaya wa Mahakama ya Ajira na Mahusiano ya Kazi jijini Nairobi wiki jana aliagiza wahusika kujadiliana na kukubaliana kuhusu huduma za kiwango cha chini kabisa zitakazodumishwa wakati wa mgomo wa madaktari ili wagonjwa wasiteseke.

TRT Afrika