Susan Nakhumicha waziri wa afya Kenya amesema serikali haina rasilimali  ya kulipa madakitari wapya waliofuzu mafunzo/  Picha kutoka Wizara ya afya Kenya 

Muungano wa Madaktari, Wafamasia na Madaktari wa Meno nchini Kenya, KPMDU, umetoa notisi ya mgomo ya siku saba, ambayo itaisha usiku wa manane wa tarehe 13 Machi 2024.

Madaktari na wataalamu wengine wa afya wanaitaka serikali kutimiza mahitaji yao, la sivyo wataweka vifaa vyao vya kazi chini.

Masuala muhimu yaliyoibuliwa na KMPDU ni pamoja na kucheleweshwa kwa kazi ya kuajiriwa hasa kwa madiktari wapya waliomaliza masomo yao.

Lakini serikali imesema haina pesa.

“Kwa sasa jambo hilo si endelevu, kama Wizara hatuna nyenzo na sheria haituruhusu kama Wizara kutangaza wakati hatuna bajeti,” alisema Waziri wa Afya Susan Nakhumicha.

Madaktari pia wanadai kuwa wanataka kurejeshwa kwa makato ya ushuru wa nyumba yaliyofanyika katika mishahara yao, ambayo mahakama ilitangaza kuwa kinyume na katiba.

Pia wanalalamikia uhaba wa bima ya matibabu ya serikali, na kaunti tofauti kukosa ajira kwa madaktari ilihali kulikuwa na makubaliano ya ajira tangu 2019.

Muungano huo pia ukosoa kandarasi duni za madaktari walioajiriwa, kushindwa katika ugawaji wa bajeti ya mafunzo tangu 2019, na tofauti za manufaa kama vile mikopo ya magari kwa wafanyakazi wengine wa umma.

"Tulienda wizarani, na cha kusikitisha hakuna kitu cha maana kilichotoka katika mkutano huo. Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya alisema kwamba wafanyakazi wa mafunzo ya udaktari wasubiri hadi Julai au wakubali kufanya kazi bila mshahara," Dennis Miskellah, Katibu Mkuu wa KMPDU alisema.

Wakenya tayari wameanza kuonyesha hofu yao kuhusu mgomo huo uliopangwa wiki ijayo, wengine wakidai kuwa itakuwa hatari kwa maisha ya watu wanaohitaji huduma za afya.

TRT Afrika