Meli za jeshi la wanamaji la Uchina (PLA) zikiongozwa na meli kubwa aina ya Destroyer kwa jina Nanning, zimetia nanga katika pwani ya Nigeria kwa ziara nadra ya jeshi la China katika pwani ya Afrika ya Atlantiki, ambapo Beijing imekuwa ikifanya jitihada za kuongeza ushawishi wake kwa muda mrefu.
Balozi wa China nchini Nigeria ameipongeza ziara hiyo ya siku tano kuwa ni hatua muhimu katika uhusiano baina ya nchi hizo mbili.
''Jeshi la wanamaji la Nigeria limeelezea nia ya kufanya kazi na China ili kukabiliana na vitisho vya usalama wa baharini na kudumisha utulivu katika Ghuba ya Guinea,'' ubalozi wa China ulisema katika taarifa yake siku ya Jumatatu.
Afrika Magharibi yenye utajiri wa mafuta ni msafirishaji muhimu wa kimataifa wa mafuta ghafi huku Nigeria ikiwa muuzaji mkuu.
Mtafiti mkuu na mzalishaji wa mafuta wa China CNOOC Ltd anajishughulisha na uzalishaji katika bahari kuu katika pwani ya Nigeria.
Mwezi Januari, Nigeria ilifungua bandari ya kina yenye thamani ya mabilioni ya dola iliyojengwa na Wachina huko Lagos.
Bandari mpya ya bahari kuu ya Lekki ni mojawapo ya bandari kuu katika eneo hilo. China imepanua ushawishi wake wa kiuchumi na kijeshi barani Afrika katika miaka ya hivi karibuni.