Kila msanii ana angalau mtindo mmoja unaowatambulisha bele ya macho ya umma.
Mbinu hiyo mahususi ambayo hufanya kazi ya ubunifu kuwa ya kipekee na kutambulika papo hapo ni mtindo wa sahihi wa msanii.
Baadhi ya wasanii hutumia mitindo tofauti maishani mwao, huku wengine, kama vile msanii wa Uhalisia kutoka Nigeria John Adenuga Opeyemi, mara nyingi huchanganya mitindo ili kukuza ubunifu.
"Hyperrealism" ni aina ya uchoraji inayofanana na picha halisi zenye mwonekano wa juu.
Kazi ya sanaa ya kuvutia
Opeyemi, ambaye huunda mchoro wa kuvutia, anasema msukumo wa kutia rangi nzito katika sanaa yake ulichochewa na hamu ya kuakisi utamaduni wa Kiafrika.
"Kila kitu katika picha zangu za uchoraji kuanzia mwonekano wa wanamitindo hadi mavazi yao inahusisha mambo ya kitamaduni ya Kiafrika," John anaiambia TRT Afrika. "Huo ndio utambulisho wangu. Hivyo ndivyo nilivyo."
Picha nyingi za John zinaonekana kutokamilika, ishara dhahiri kwa mtu yeyote anayetazama mchoro wake ajaze sehemu zilizowachwa, na hivyo kufanya michoro yake kuwa na mvuto kisaikolojia. Na hivyo kufanya picha zake za uchoraji kuwa za kusisimua zaidi.
"Wakati mtu anapo hangaika, uwezo kamili wake haufichuiki kila mara. Hii ndiyo sababu ya kutochora picha kamili, ili kuashiria mustakabli na ile sehemu iliyo kamilika kuashiria muda wa sasa," John aeleza.
"Kivuli kwenye picha, kwa upande mwingine, ni taswira ya siku za nyuma kwangu na mamilioni ya Waafrika wanaohangaika na kujitahidi kufikia malengo yao."
Mapenzi ya utotoni
Kuvutiwa kwa John na sanaa kulianza utotoni. Katika shule ya upili, alikuwa akichora michoro ya masomo yake ya sayansi kwa usahihi, hadi kwamba walimu wake mara nyingi walikuwa wakimwomba achore ubaoni wakati wa masomo.
"Nilikuwa nikitazama mafunzo tofauti kwenye YouTube ili kupata vidokezo juu ya "hyperrealism" na kukuza mbinu yangu mwenyewe," anasema John.
Baadaye alisomea sanaa ya ustadi katika Chuo Kikuu cha Benin ambapo alianza kufanya majaribio ya rangi nzito, akichanganya rangi na penseli na hatua kwa hatua akatengeneza mtindo wake anayotumia hadi sasa.
Kabla ya kuanza uchoraji, John kwanza anaandika nukta kadhaa kwenye daftari kabla ya kuamua atakachokichora. Hatua inayofuata ni kuunda fikra na kuchagua rangui ya kutumia.
Sanaa yenye 'Sauti'
Amefanya kazi na wanamitindo waliobobea, lakini wengi wa watu wanaojitolea kutumiwa kama modeli ni marafiki zake, majirani na hata watu wasiowafahamu wanaokubali kumruhusu awapige picha kwenye studio yake iliyoko Jijini Benin.
Baadaye, anachagua picha bora zaidi za kuchora. Mojawapo ya michoro yake ya hivi majuzi ni mkusanyiko unaoitwa "Upendo, Amani na Udanganyifu" unaoangazia wanamitindo wanaoonekana kuruka juu ya turubai akitumia mchor wa aina ya "hyperrealism".
"Nataka ujumbe wa sanaa yangu usikike. Kazi iliyokamilika inapaswa kuonyesha hisia ninazotaka kuonyesha," msanii huyo mwenye umri wa miaka 31 anasema. "Kupitia michoro hii, nia yangu ilikuwa kuwasilisha ujumbe wa upendo, amani, maisha bora, ambayo Waafrika wengi wanatamani."
Kila moja ya sehemu ya michoro huchukua kama muda wa wiki tatu kukamilika.
Zawadi ya thamani
John anakadiria kuwa amefanya angalau kazi za sanaa 700 zilizoagizwa na watu tangu aanze uchoraji wa kitaalamu mnamo 2017.
Mara nyingi yeye hujaribu kuchora picha zake binafsi, aina ya sanaa ambayo wasanii wengi wanaona vigumu kufanya. Kujipeleleza katika kuchora kwa kina mara nyingi husumbua wasanii wengine.
Lakini John anafurahia kuchora picha za kibinafsi. Safari yake ya kujipiga picha ambayo ilianza miaka kadhaa iliyopita ikawa utamaduni wa aina yake.
"Nilianza kuchora picha zangu mwenyewe kila mwaka ili kuadhimisha siku yangu ya kuzaliwa. Ni jambo ambalo naona linanivutia kwa sababu kila mstari na alama kwenye uso wangu ni hadithi ya safari ya maisha yangu," anasema. "Kwa muda mrefu, hiyo ndiyo ilikuwa zawadi pekee yenye thamani ambayo ningeweza kujitolea."
Uzuri wa Afrika
Sanaa mbalimbali za John zimeonyeshwa katika majumba ya maonyesho kote Nigeria, Ufaransa na Marekani.
Safari yake ya kutambulika kitaifa na kimataifa hata hivyo haijakuwa bila na changamoto.
"Sanaa kwa bahati mbaya haithaminiwi katika sehemu nyingi za Afrika. Inaweza pia kukatisha tamaa sana wakati mchoro wa Kiafrika ambao ulichukua wiki kadhaa kuundwa unapunguzwa bei," anasema.
Hata hivyo, ana matumaini kwamba kuongezeka kwa idadi ya majumba ya sanaa duniani kote yanayoonyesha sanaa ya Kiafrika kutaongeza ari miongoni mwa wasanii wengi wachanga kama yeye.
"Ninajaribu kuonyesha sanaa yangu kwa ulimwengu wote ili kuwafahamisha kuwa utamaduni wetu wa Kiafrika ndio urembo wa Kiafrika," anasema.