Rais wa Kenya William Ruto ameteua jopo la watu tisa walio na jukumu la kuwasaili na kuwachuja watakaokuwa kwenye nafasi za Uenyekiti na makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
Uteuzi huo unafuatia uamuzi wa Ijumaa iliyopita wa Mahakama Kuu, ambao uliondoa amri za awali za mahakama zilizokuwa zimezuia uteuzi wao.
Maafisa hao tisa tayari wameapishwa katika hafla fupi iliyofanyika Mahakama ya juu ya nchi.
Jaji Mkuu Martha Koome akiwaapisha alisema jukumu la jopo hilo katika kuunda IEBC ni muhimu kwa mustakabali wa nchi.
" Uwazi katika uchaguzi ndio unaobainisha uthabiti na hatima ya taifa letu. Historia imetuonyesha kuwa uchaguzi unapokuwa huru, wa haki, na wa uwazi taifa letu hustawi. Kwa hivyo, Jopo la Uteuzi lina jukumu kubwa zaidi la kuchagua wanaume na wanawake wenye uadilifu na uaminifu wa kuongoza IEBC." Jaji koome alisema.
" Ninahimiza taasisi na wadau wote wanaohusika katika mchakato huu - bunge, wanasiasa, mashirika ya kijamii, na umma - kuhakikisha kuwa uteuzi wa Makamishna wapya wa IEBC unafanywa kwa kasi, uadilifu, na uwazi. Wananchi wa Kenya wana matumaini na wanatakiwa wapate matokeo yaliyopitia mchakato wa hali ya juu," Jaji Koome aliongeza.
Jaji Mkuu Koome amesema IEBC sio tu taasisi nyingine ya serikali; ni mhimili wa uadilifu wa uchaguzi, na muundo wake lazima uonyeshe viwango vya juu vya taaluma na uwazi.
Julai 2024, Rais William Ruto aliidhinisha Muswada wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na kuweka mazingira ya kuteuliwa kwa Mwenyekiti na Makamishna wa tume kabla ya uchaguzi wa Kenya 2027.
Oktoba 2024, Mahakama ya Juu nchini Kenya ilisitisha uundaji upya wa tume ya uchaguzi nchini Kenya, ikizuia uwasilishaji wa majina kutoka kwa kamati ya uteuzi ya IEBC hadi kwa Rais William Ruto ili kuidhinishwa.
Uamuzi huo ulifuatia pingamizi la kisheria la Boniface Njogu, ambaye aliibua wasiwasi juu ya ushirikishwaji wa mchakato wa uteuzi. Miongoni mwa madai yake ilikuwa kwamba uteuzi wa serikali unatakiwa kuzingatia kifungu cha katiba kuwa angalau asilimia tano ya wanachama wa kamati za umma iwe ni watu wenye ulemavu.
Mahakama hiyo sasa imeondoa vikwazo hivyo.