Benki kuu ya Rwanda inaripoti kuongezeka kwa uwekezaji wa moja kwa moja wa Kigeni. Serikali inasema mnamo 2021, ilivutia uwekezaji wa thamani ya takriban dola za Marekani milioni 399.3, ikilinganishwa na dola za Marekani milioni 274. lililorekodiwa mnamo 2020.
Ripoti ya sensa ya Mitaji ya Kigeni (FPC) ya 2022, inasema Mauritius, Kenya, Afrika Kusini, Marekani na India vilikuwa vyanzo vikuu vya hisa za mapato hayo.
Ripoti ya benki hiyo inasema " Kupanda kwa mapato kunaweza kuhusishwa na kufufuka kwa shughuli za kiuchumi kutokana na utendaji duni uliosababishwa na janga la Uviko au COVID-19 mwaka 2020."
Je ni sekta gani nchjini Rwanda zilizovutia uwekezaji?
Takwimu zaonyesha kuwa mwaka 2021, sekta ya fedha ilivutia mapato ya juu zaidi ya dola za Kimarekani milioni 155.3, ikifuatiwa na utalii yenye dola za Kimarekani milioni 87.9 , ujenzi ilivutia dola milioni 68.4 na viwanda vikavutia dola milioni 63.8 milioni.
Ongezeko la mapato kutoka sekta ya utalii linaonyesha kuimarika kwa sekta hii baada ya kushuka kwa kasi mwaka wa 2020, kutokana na vikwazo vya usafiri vilivyowekwa na nchi ili kupunguza kuenea kwa janga kubwa la Uviko-19.
Rwanda inawekeza fedha nyingi katika michezo kupitia ushirikiano na vilabu kama vile Arsenal na PSG .
Mabango yalioandakiwa "Tembelea Rwanda" sasa yanaweza kuonekana kwenye viwanja vya Ligi kuu ya soka na Ligue 1.
Pia imeandaa mashindano ya dunia ya baiskeli za barabarani.
Rwanda pia inawekeza katika uwekezaji wa afya.
Kampuni ya bioteknolojia ya Ujerumani, BioNTech inajenga kiwanda chake cha kwanza cha kutengeneza chanjo Kigali, Rwanda ambayo itauzwa kote barani Afrika.
Hivi majuzi inesaini maakubaliano na Umoja wa Afrika kujenga makao makuu ya Shirika la Madawa la Afrika (AMA).
Shirika hili la Afya la bara limepewa jukumu la kuongeza ufikiaji wa bidhaa za matibabu ambazo ni za kuaminika, za ufanisi, za gharama nafuu, na za ubora wa juu katika mataifa yote ya Afrika.
Ripoti hiyo inapendekeza kuwa ili kuboresha uwezo wa uwekezaji wa nchi, serikali ya Rwanda inapaswa kuendelea kutoa motisha kwa wawekezaji wa ndani na nje kupitia bodi ya maendeleo ya Rwanda.
Hata hivyo katika ukanda wa afrika mashariki Rwanda imekuwa ikiwekeza katika sekta ambazo zinaonekana ngumu huku mara kwa mara wakiboresha sera zao za biashara na uwekezaji