Na Edward Qorro
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Dunia inapitia mabadiliko ya kasi, kuna dhana kuu moja ambayo inatawala mabadiliko haya.
Japo haizungumziwi sana ndani ya bara la Afrika, ni ukweli usiopingika kuwa 'Akili Mnemba,' au Akili Bandia kama inavyojulikana na wengi ina faida nyingi kuliko hasara kwa vijana, wakati bara la Afrika linapojiandaa kuipokea dhana hii kwa asilimia mia moja.
Katika dhana rahisi sana, Akili Bandia ni mwigo tu wa michakato ya akili ya binadamu kwa kutumia mashine. Hapa tunatumia kompyuta kuchakata kiasi kikubwa cha taarifa inayotolewa na binadamu ili kutoa matokeo yenye mifumo na vipengele sawa na vile ambavyo binadamu angefanya. Akili Bandia inaweza kutumika katika nyanja tofauti na kwa madhumuni tofauti.
Kwa uvumbuzi wa kila siku hasa kwenye 'AI generative,' teknolojia hii inaweza kutumika katika usindikaji wa lugha asilia, mifumo ya wataalamu, utambuzi wa usemi na maono ya mashine. Kitaalam, Akili Mnemba inatakiwa kuboresha shughuli za binadamu na si vinginevyo.
Mnamo Machi 2023, mwezi mmoja baada ya kuanzishwa kwa Akili Bandia maarufu kama ChatGPT inakadiriwa ina zaidi ya watumiaji milioni 100 wanaotumia teknolojia hii kila mwezi.
Tishio kwa ajira
Wakati Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) inakadiria kuwa takriban vijana milioni 100 barani humu watakosa kazi kufikia mwaka 2030 kutokana na maendeleo ya Teknolojia. Wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wanasema kuna faida nyingi zinazopatikana kutokana na uwepo wa 'Akili Mnemba' kuliko faida zake.
Hata hivyo, wanaonya kwamba watakaonufaika zaidi ni vijana wabunifu na 'wenye kujiongeza' na sio wavivu.
"Kwa vijana wavivu na wasio na ubunifu, bila shaka dhana hii itakuwa tishio kwao kwani itachukua kazi nyingi rahisi ambazo walikuwa wanazifanya hapo awali. Wale wabunifu, hii itakuwa ni fursa ya kuvumbua bidhaa na huduma mpya ambazo zitaendeshwa sana na dhana hii," Nuzulack Dausen, Afisa Mtendaji Mkuu wa Nukta Afrika, kampuni ya Teknolojia inayojihusisha na vyombo vya habari vya kidijitali, anaiambia TRTAfrika.
Kulingana na Dausen, ushahidi wa manufaa ya dhana hii unaonekana kwenye uwepo wa makampuni ya Kiafrika, na kwa namna ya kipekee Tanzania, yanayoongozwa na vijana kama vile Sarufi AI ambayo yametengeneza modeli za lugha zinazosaidia wafanyabiashara kuwasiliana papo hapo na wateja wao.
Nuzulack Dausen, Afisa Mtendaji Mkuu wa Nukta Afrika
"Nionavyo mimi, wakati wa kutawaliwa na Akili Bandia utakuwa ni wa kufurahisha zaidi na wa kutisha," anaongeza.
Uyatari wa Bara la Afrika
Wakati mataifa mengi Ulaya, yapo mbioni kuandaa sera na miongozo ya matumizi ya 'Akili Mnemba' kwenye matumizi yao ya kila siku, bado safari inaonekana kuwa ni ndefu kufikia hatua hiyo kwa bara la Afrika.
"Nina wasiwasi hapa kutoa jibu la mabano ikiwa Afrika imejiandaa au la. Hata hivyo, tumeona nchi kadhaa zimeanza kukubaliana na dhana hii katika sekta tofauti," anasema Dausen.
Hata hivyo, kulingana na mtaalamu huyo, tofauti na nchi za Ulaya ambako maendeleo na hatua kubwa zimefanyika kutekeleza dhana hii, itachukua muda mrefu kidogo kwa bara la Afrika kuingia kwenye mfumo huu mpya, hasa ukizingatia changamoto za kimiundombinu na rasilimali fedha zinazoikumba nchi nyingi za Afrika.
Dausen anasema kuwa matumizi ya huduma za kimtandao katika nchi nyingi za Afrika bado yako chini, huku kukiwa na idadi ndogo ya wamiliki wa vifaa vya kielektroniki kama vile 'simu janja' bila kusahau kukatika kwa mara kwa mara kwa umeme.
Katika ripoti yake ya robo ya nne ya mwaka 2023 iliyotolewa hivi karibuni, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inasema kuwa ni asilimia 32.13 tu za simu hizo za kisasa ziko katika matumizi nchini humo.
"Hadi kufikia Disemba 2023, matumizi ya simu zote yamefikia asilimia 85.62, lakini yale ya simu janja yameongezeka kutoka asilimia 30.71 hadi kufikia 32.13," inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Kulingana na mdhibiti huyo wa huduma za mawasiliano nchini Tanzania, asilimia 67.8 ya watanzania waishio mijini wanapata huduma za intaneti ukilinganisha na asilimia 28.9 ya waishio maeneo ya vijijini.
Gharama kubwa
Dausen anasema kuwa ni gharama sana kuanzisha mifumo mikubwa ya 'Akili Mnemba' ana amini kuwa miradi hiyo inahitaji pesa nyingi ili siku moja Afrika nayo iweze kujivunia mifumo kama CHAT GPT na Gemini.
"Miondombinu iliyopo inaibua maswali mengi kuhusu utayari wetu, pia kuna chache sana zinazowekeza kwenye teknolojia hii," anaielezea TRTAfrika.
"Hata hivyo, nina matumaini kuwa watu wengi watatumia zana zilizo tayari kwa ajili ya manufaa yanayotegemewa."