Katika karne ya 21 kumekuwa na ongezeko la chuki dhidi ya Waislamu katika mataifa ya Magharibi, ambayo pia yamejaribu kulazimisha utamaduni wa Magharibi kwa watu, na kuchagua upande wanaounga mkono katika vurugu na mizozo duniani.
Cha kushangaza ni kuwa wanadiplomasia wa Kiislamu wameziba pengo hilo na wameonesha kuwa wanaongoza juhudi za upatikanaji wa amani duniani.
Kufuatia juhudi za majadiliano yaliyoratibiwa na Uturuki, raia watano wa Thailand waliachiliwa huru hivi karibuni na Hamas huko Gaza. Huu ulikuwa mfano wa hivi karibuni wa taifa la Kiislamu kuongoza juhudi muhimu za kidiplomasia na kujaza ombwe lilioachwa na Marekani na washirika wake wa Magharibi.
Chini ya miezi miwili iliyopita, mwezi Disemba, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alitangaza "upatanisho wa kihistoria" kati ya Ethiopia na Somalia kufuatia mazungumzo ya amani yaliyoratibiwa na Uturuki.
Mwaka 2022, Uturuki ilikuwa mwenyeji wa mazungumzo ya amani ya Istanbul, ambayo yalikuwa karibu kumaliza vita vya Ukraine mwezi mmoja tu baada ya vita hivyo kuanza, lakini Marekani na Uingereza wakawa kizingiti wa jitihada hizo.
Uturuki iliwaleta Urusi na Ukraine pamoja na kukubaliana kuhusu usafirishaji wa nafaka na chakula kutoka Ukraine, bidhaa hizo pamoja na mbolea zilikuwa zinahitajika zaidi katika maeneo mbali ikiwemo mataifa yanayoendelea duniani.
Nchi zingine za Kiislamu zinajitahidi kutimiza majukumu yao. Kwa pamoja, Saudi Arabia na Uturuki walifanikiwa kusaidia kuachiwa huru kwa wafungwa wa mataifa ya Magharibi kutoka Urusi Septemba 2022.
Saudia Arabia ilikuwa wenyeji wa mkutano wa kwanza wa amani kuhusu Ukraine jijini Jeddah 2023. UAE pengine imekuwa na jukumu kubwa katika kusaidia kuachiliwa huru kwa wafungwa wa Urusi na Ukraine na makabidhiano ya miili ya wale waliokufa vitani.
Hivi karibuni Qatar ilihusika katika makubaliano ya kwanza ya kusitisha mapigano Gaza na inasemekana kuwa wenyeji wa mazungumzo ya hatua za mwanzo kati ya maafisa wa Urusi na Ukraine yaliyolenga kumaliza vita vya miaka mitatu.
Kwa miaka mingi, Qatar imekuwa kitovu cha majadiliano kati ya Marekani na Taliban kabla mataifa ya Magharibi kuyumba katika kuondoa watu wao kutoka Afghanistan 2021.
Chuki dhidi ya Uislamu na mataifa ya Magharibi
Mchango mkubwa wa uongozi katika diplomasia ya Waislamu ni tofauti na kuongezeka kwa chuki dhidi ya Uislamu katika karne hii ya ishirini na moja.
Chuki dhidi ya Uislamu hazijaanza 2001, lakini mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11 jijini Washington DC ilichochea chuki zaidi nchini Marekani na katika mataifa ya Magharibi.
Wanaoeneza chuki dhidi ya Uislamu wanatumia mbinu mbaya na za kuumiza kuharibu sifa za Waislamu, mara nyingi zikifanywa na wafuasi wa mrengo wa kulia wanaopotosha taarifa. Katika wiki ambayo mashambulio ya 9/11 yalitokea, watu watatu waliuawa nchini Marekani, mmoja wao alikuwa Singasinga, aliyeuawa kwa risasi kwa kufananishwa na mhamiaji wa Kiislamu kwa sababu ya rangi yake na ndevu.
Mambo haya bado yanaendelea hadi leo. Ripoti kutoka shirika la Pew Centre zinaonesha viwango vya uhalifu vya chuki dhidi ya Waislamu nchini Marekani vya 2016 vimezidi vile vya 2001. Baada ya vita kuanza kwa vita vya Hamas na Israeli Oktoba 2023, chuki zilizidi.
Bila shaka chuki dhidi ya Uislamu zilichochea na kuongeza kuungwa mkono kwa mipango ya Marekani ya vita dhidi ya ugaidi duniani vilivyoanza baada ya 9/11, kwanza walivamia Afghanistan na pili vita vya Iraq 2003.
Vita hivi vinakadiriwa kugharimu Marekani dola trilioni $8 na kusababisha vifo vya watu 900,000, wengi wakiwa hawana hatia.
Ilisababisha washukiwa kuanza kutekwa katika mataifa ya kigeni na kupelekwa katika vituo vya kuzuiwa watu vya Marekani kwa ajili ya kuhojiwa na kushtakiwa. Mwaka 2008, serikali ya Uingereza ililazimika kuomba radhi kwa kuhusika na kusaidia Marekani katika utekaji huo.
Chuki dhidi Uislamu zinaonekana kutawala siasa za Uingereza. Katika siku za nyuma wanachama wa chama tawala cha Uingereza cha Leba kimeshutumiwa kwa chuki dhidi ya Uislamu.
Chama cha Uingereza cha Conservative – ambacho kimekuwa madarakani 2010 hadi 2024 – kililazimika kuomba radhi 2021 wakati utafiti huru ulipobaini kuwa “chuki dhidi ya Waislamu bado ni tatizo”.
Ulimwenguni, mataifa ya Kiislamu yanashtumiwa kwa kuwa na siasa ambazo haziheshimu demokrasia na madai ya kukiuka haki za binadamu.
Madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu na ukosefu wa demokrasia ndiyo yanayotumiwa na maafisa wa Ulaya kuinyima Uturuki nafasi ya kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya.
Ni Uturuki ambayo ilisaidia pakubwa kukuza uchumi wa Ujerumani Magharibi, licha ya kuwa kuwepo kwao chini ya mfumo wa wafanyakazi wa kigeni kulikuwa katika mazingira mabaya ya kufanyishwa kazi nyingi na kubaguliwa kwa misingi ya rangi.
Kutoka kwa nyota wa tasnia ya burudani Sporty Spice hadi Rod Stewart, nyota hawa wa mataifa ya Magharibi na wenye ushawishi mkubwa walikuwa wanakashifu uandaaji wa fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar 2022.
Ni kawaida kwa vyombo vya habari vya Magharibi kuzungumzia uwekezaji wa mabilioni ya madola wa Saudia Arabia katika michezo kama njia moja ya kujipa muonekano tofauti dhidi ya madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu – wanaitaja kupoteza dira kwa kutumia michezo – au kuficha athari za uharibifu wa mazingira kutokana na shughuli za kuchimba mafuta.
Mataifa ya Kiislamu yanafananishwa na utawala unaosemekana kuwa wa kidikteta kama China na Urusi muelekeo unaothibitisha kuwa yako sawa, hayana-Umagharibi, zaidi, hayazingatii- Ukristo, na kwa hivyo hayavutii.
Raia wa Magharibi wanakwazwa na juhudi za serikali za kutaka kuendeleza kuwepo kwa uwakilishi wa watu mbalimbali, ujumuishaji na usawa.
Pamoja na hayo, taarifa za kuangazia mataifa ya Kiislamu vibaya hazina misingi yoyote ya kitamaduni wala mtazamo wa dini usio na ubaguzi, wala hakuna jitihada za kufanya Waislamu wajione kama ni sehemu ya Uingereza au maeneo mengine.
Undumakuwili wa mataifa Magharibi
Neno jipya limeingia katika misamiati ya Magharibi kwa zaidi ya miaka ishirini iliyopita.
Kuna sheria ambazo hazijabainishwa au kutolewa maelezo katika nyaraka kama ya kanuni za Umoja wa Mataifa 1945, ambazo zinahitaji kuwepo kwa amani, heshima na usawa katika dunia.
Badala yake Diplomasia ya mataifa ya Magharibi inaangazia zaidi kupata washindi katika migogoro ya kimataifa.
Sheria za kutoa muelekeo wa kimataifa ni neno linalotumika na kundi dogo la mataifa ya Magharibi ambalo halizingatii utaratibu wowote, likiongozwa na Marekani, kuamua taifa gani “liko na sisi au liko dhidi yetu”, kwa maneno ya George W Bush.
Katika karne hii ya 21 mataifa ya Magharibi yenye uwezo yameacha kufuata mfumo wa kidiplomasia unaokubalika.
Uingereza na Umoja wa Ulaya hawaonekani kuwa na nia njema. Badala yake wamekataa majadiliano, na kuangazia tu ushindi wa upande wanaoutaka dhidi ya wasiyemtaka.
Kama tunavyoliona hili kati ya vita vya Ukraine na Urusi, huku mataifa ya Magharibi yakiamini kuwa ushindi wa Ukraine ni bora zaidi kwa hali ya amani iliyo tete.
Na kwa mauaji ya halaiki ya Israeli huko Gaza, ambayo yamesababisha vifo vya watu wasiyo na hatia zaidi ya 48,000, Marekani na Uingereza, hasa wamekuwa hawana msimamo, katika kumkabili Netanyahu ambaye ni hatari kwa usalama.
Bila shaka, Rais mpya wa Marekani Trump amejaribu kumkingia kifua Netanyahu asiwajibishwe na mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai na kumtishia yoyote ambaye anataka kumshtaki Waziri Mkuu wa Israeli.
Kutokana na ombwe la mataifa yenye kutoa muelekeo duniani, nchi za Kiislamu zimeziba pengo hilo.
Ni sadfa ilioje kwamba baada ya miongo miwili ya kuongezeka kwa chuki dhidi ya Uislamu na kwa nchi za Magharibi kutofwata diplomasia inayokubalika, Wanadiplomasia wa Kiislamu ndiyo wanaoibuka kuwa wanaotafuta amani duniani.
Mwandishi wa makala haya, Ian Proud ni mwanadiplomasia wa zamani wa Uingereza na mwandishi wa kitabu 'A Misfit in Moscow: How British Diplomacy in Russia Failed.'
Kanusho: Maoni haya ya mwandishi sio msimamo, muelekeo na sera za uhariri za TRT Afrika.