Rais Donald Trump pia amelalamikia WHO kushindwa kupitisha mageuzi yanayohitajika haraka na kutokuwa na uwezo wa kuonyesha uhuru kutoka kwa ushawishi usiofaa / Picha: Reuters

Rais wa Marekani Donald Trump baada ya kuapishwa alitia saini amri ya kuiondoa Marekani katika uanachama wa Shirika la Afya Duniani, WHO.

"Marekani ilipendekeza kujiondoa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2020 kwa sababu ya Shirika hilo kushughulikia vibaya janga la Uviko-19 ambalo liliibuka kutoka Wuhan, China, na shida nyengine za kiafya za ulimwengu," Agizo la Trump linasema.

Rais Trump pia ameilalamikia WHO kushindwa kupitisha mageuzi yanayohitajika haraka na kutokuwa na uwezo wa kuonyesha uhuru kutoka kwa ushawishi usiofaa wa kisiasa wa nchi wanachama wa WHO.

"WHO inaendelea kudai malipo yenye kutaabisha isivyo haki kutoka Marekani, mbali na uwiano na malipo yaliyotathminiwa ya nchi nyingine. China, yenye idadi ya watu bilioni 1.4, ina asilimia 300 ya wakazi wa Marekani, lakini inachangia karibu chini ya asilimia 90 ya WHO," imesema.

Amesema Marekani inakusudia kujiondoa kutoka kwa WHO. Amebatilisha barua ya Rais kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa iliyotiwa saini Januari 20, 2021, ambayo ilibatilisha ombi la Marekani la Julai 6, 2020.

Rais Trump kwa amri yake amesema Marekani itasitisha kutoa fedha, usaidizi au rasilimali za serikali ya Marekani kwa WHO.

Serikali pia imeamrishwa na Rais Trump kuwarejesha na kuwapa kazi upya wafanyakazi wa serikali ya Marekani au wakandarasi wanaofanya kazi katika nafasi yoyote WHO.

Serikali ya Marekani sasa itatafuta washirika wa kimataifa wanaoaminika na wenye uwazi ili kuchukua shughuli muhimu zilizofanywa hapo awali na WHO.

TRT Afrika