Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud pamoja na Rais Isaias Afwerki wa Eritrea na Rais Abdel Fattah El-Sisi wa Misri walishiriki katika Mkutano wa Nchi Tatu huko Asmara, Eritrea. / Picha kutoka Villa Somalia

Rais Abdel Fattah El-Sisi wa Misri na Rais Mohamud Sheikh wa Somalia wapo nchini Eritrea kufuatia mwaliko wa Rais wa Eritrea Isaias Afwerki.

"Ziara hiyo itajikita katika kujadili njia za kuimarisha mahusiano baina ya nchi hizo katika nyanja mbalimbali, pamoja na kushughulikia juhudi za hali ya kikanda za kuweka utulivu na usalama katika Pembe ya Afrika na Bahari ya Shamu, kwa namna ambayo inaunga mkono maendeleo na kuhudumia maslahi ya nchi, " tovuti ya Ikulu ya Misri imesema.

Rais el-Sisi, alikuwa na viongozi waandamizi, akiwemo Waziri wa Usalama wa Taifa na Waziri wa Mambo ya Nje, alipopokewa na Rais Isaias kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Asmara.

Ziara ya El-Sisi inafuatia kuwasili kwa Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud, Oktoba 9, 2024 kwa ziara ya siku tatu.

Rais Hassan Sheikh Mohamud alishiriki katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi Tatu huko Asmara, Eritrea, pamoja na Rais Isaias Afwerki wa Eritrea na Rais Abdel Fattah El-Sisi wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri," Ikulu ya Somalia ilisema katika mtandao wake wa X.

Mazungumzo hayo yalifanyika huku kukiwa na mvutano unaoongezeka katika eneo la Pembe ya Afrika, kufuatia kutiwa saini Januari 1, 2024, kwa Mkataba wa Maelewano (MoU) kati ya Ethiopia na Somaliland, ambao unalenga kuipa Ethiopia fursa ya baharini kwa ahadi ya kuitambuwa Somaliland kama taifa.

Pia uamuzi wa Misri kutuma shehena yake ya pili ya msaada wa kijeshi nchini Somalia, ikiwa ni pamoja na silaha nzito za kivita na magari ya kivita kama sehemu ya mkataba wa ulinzi uliotiwa saini kati ya Misri na Somalia mnamo Agosti 2024, umezua wasiwasi nchini Ethiopia na Somaliland.

TRT Afrika