Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amefutilia mbali mzozo kati yake na Somalia kuhusu mpango wa kufikia Bahari Nyekundu na eneo lililojitenga la Somalia la Somaliland.
Abiy aliliambia bunge la shirikisho siku ya Jumanne kwamba Addis Ababa haina nia ya kuleta madhara kwa Somalia huku akikumbushia wanajeshi wa Ethiopia waliokufa kwa ajili ya "amani ya Somalia."
Alisema watu wa Ethiopia na Somalia "wamefungamana kwa damu ."
"Kwa hiyo, urafiki kati ya nchi hizi mbili ni mkubwa," alisema, akiongeza kuwa Ethiopia haikubali vita dhidi ya nchi yoyote "kimsingi."
Uchochezi wa nje
Uhusiano kati ya majirani hao wawili umekuwa mbaya tangu Ethiopia ilipofikia makubaliano na Somaliland Januari 1.
Lakini Abiy alisema wachochezi kutoka nje , ambao hakuwataja, wanajaribu kuchochea mzozo kati ya mataifa hayo mawili "jambo ambalo halipaswi kutokea."
Alisema ombi aliyotoa ka Somaliland la kutumia bahari ni kwa msingi wa manufaa ya pande zote mbili ambayo ni muhimu sio tu kwa Ethiopia lakini kwa ushirikiano wa kikanda.
Somalia imekataa makubaliano ya bandari ya Ethiopia ya Bahari Nyekundu na Somaliland, na kuyaita "haramu," tishio kwa ujirani mwema na ukiukaji wa uhuru wake.
Pia ilimwita balozi wake nchini Ethiopia baada ya mpango huo kutangazwa.
Serikali ya Ethiopia imetetea uamuzi wake wa kutia saini mkataba huo bila idhini ya Mogadishu, na kusema makubaliano na Somaliland "hayataathiri chama chochote au nchi."
Mpango huo unaruhusu Ethiopia kupata kituo cha kudumu na cha kutegemewa cha wanamaji na huduma ya kibiashara ya baharini katika Ghuba ya Aden.
Ethiopia ilipoteza bandari zake za Bahari Nyekundu mapema miaka ya 1990 baada ya Vita vya Uhuru wa Eritrea, vilivyodumu kutoka 1961 hadi 1991.
Mnamo 1991, Eritrea ilipata uhuru kutoka kwa Ethiopia, na kusababisha kuanzishwa kwa mataifa mawili tofauti. Utengano huo ulisababisha Ethiopia kupoteza ufikiaji wa moja kwa moja kwenye Bahari Nyekundu na bandari kuu.