Rais wa Kenya William Ruto amewasili mjini Juba, Sudan Kusini, kwa mazungumzo na Rais Salva Kiir Mayardit kuhusu mchakato wa amani uitwao Tumaini Initiative, ikulu ya Kenya imesema.
Wiki jana, Rais Ruto alifanya mazungumzo na wajumbe wa serikali kutoka Sudan Kusini na pia kukutana na wawakilishi wa vyama vya Upinzani katika Mpango wa amani wa Sudan.
"Makundi hayo mawili yamethibitisha kuwa tayari kusaini makubaliano ya Tumaini, matokeo ya mazungumzo shirikishi," Ikulu imesema.
Kenya imekuwa mwenyeji wa mazungumzo kati ya Serikali ya Mpito Iliyohusisha Umoja wa Kitaifa na makundi mengine ili kuendeleza Mkataba Uliohuishwa wa Utatuzi wa Mzozo katika Mkataba wa Amani wa Sudan Kusini wa 2018.
Sudan Kusini inajitahidi kujikwamua kutoka kwa athari ya vita vya ndani vilivyoanza nchini humo Desemba 2013 kati ya Rais wa wakati huo Salva kiir na makamu wake Riek Machar.
Zaidi ya muongo mmoja wa mapigano yamesababisha Sudan Kusini kukumbwa na mojawapo ya mizozo mikubwa zaidi ya wakimbizi barani Afrika.
Zaidi ya raia milioni 4 wamelazimishwa kukimbia makwao. Zaidi ya milioni 2.2 wameondoka nchini kabisa, wakati wengine milioni 2.2 wamehamishwa ndani.
Na sasa wengi waliokimbilia nchi jirani ya Sudan wanalazimika kurudi tena nyumbani kwani Sudan sasa imekumbwa na vita vya ndani.
Mpango wa amani wa Tumaini Initiative
Mpango wa amani wa Tumaini Initiative, ulizinduliwa na Rais Salva Kiir Mayardit wa Sudan Kusini baada ya kubaini kuwa mpango wa amani wa Roma, uliopatanishwa na Sant Egidio wa Kanisa Katoliki, haukuleta tija.
Jukwaa hilo, lililojumuisha Serikali ya Sudan Kusini na vikundi vya waasi waliopinga Mkataba Uliohuishwa wa Utatuzi wa Mzozo wa Sudan Kusini wa 2028, lilikuwa likiendelea tangu 2020 , bila kufikia matokeo yoyote thabiti.
Mnamo Mei 2024, Rais Salva alimwomba Rais William Ruto wa Kenya kupatanisha mzozo kati yao na Ruto akakubali.
Mpango wa maongezi ya amani yakaitwa "Tumaini Initiative " na yalianza Nairobi mnamo Juni 2024.
Mpango huu hadi sasa umehitimisha mazungumzo kuhusu itifaki tisa, nyingi zikiwa na lengo la kutatua migogoro ya kudumu huku pia ikianzisha taasisi thabiti za kuwalinda watu wa Sudan Kusini.