Mkutano wa Urusi na Afrika ulifanyika 27 na 28 Julai nchini Urusi / Picha: AFP

Viongozi wa Afrika walimsisitizia rais wa Urusi Vladimir Putin siku ya Ijumaa kuwa kuna umuhimu wa kurudishwa amani kati yake na Ukraine. Nchi hizo mbili zimekuwa na mzozo tangu Februari mwaka huu.

Pia walimtaka Putin kufanya upya mkataba muhimu kwa Afrika kuhusu usafirishaji salama wa nafaka za Ukraine huku vita vikiendelea . Moscow ilijitoa katika mkataba huo.

Rais wa Jamhuri ya Kongo Denis Sassou Nguesso aliambia rais Vladmir Putin kuna umuhimu wa amani kurejea haraka baina yake na Ukraine  /Picha AFP

"Vita hivi lazima viishe. Na vinaweza tu kumalizika kwa misingi ya haki na uelewano," Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat aliwaambia Putin na viongozi wa Afrika huko St Petersburg.

"Mpango wa nafaka lazima uendelezwe kwa manufaa ya watu wote duniani, hasa Waafrika."

Afrika inataka mzozo wa Urusi na Ukraine kumalizika haraka iwezekanavyo / Picha : AFP

Putin alitoa mapokezi mazuri wakati viongozi wa Afrika walipowasilisha kwake ujumbe wa amani mwezi uliopita.

Katika hotuba yake siku ya Ijumaa, alirejelea hoja yake kwamba ni Ukraine na nchi za Magharibi, sio Urusi, ndizo zinazosababisha kuendelea kwa mzozo.

Rais wa Jamhuri ya Kongo Denis Sassou Nguesso alisema mpango huo "unastahili kuangaliwa kwa karibu zaidi", akitoa wito wa "haraka" wa amani.

Rais Yoweri Museveni wa Uganda ni kati ya viongozi wa Afrika walio katika kamati ya upatanishi dhidi ya vita kati ya Ukraine na Urusi / Picha: AFP 

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alimwambia Putin: "Tunahisi kwamba tuna haki ya kutoa wito wa amani - mzozo unaoendelea pia unatuathiri vibaya."

Wito huo ulimfanya Putin mara kwa mara kutetea msimamo wa Urusi na hatimaye kutoa taarifa ya dakika nane, ambayo baadaye ilitolewa na Kremlin kwenye video, mwanzoni mwa mazungumzo ya jioni na viongozi wa Afrika nyuma ya mpango wa amani.

Umoja wa Afrika umeitaka Urusi kuhakikisha nchi za Afrika zinaendelea kupata nafaka kutoka ukraine / Picha :AFP

Urusi kwa muda mrefu imesema iko tayari kwa mazungumzo lakini ni lazima yazingatie "ukweli mpya" uliopo.

Mwenyekiti wa AU Azali Assoumani alisema Putin ameonyesha utayari wake wa kuzungumza, na "sasa inabidi tushawishi upande mwingine".

Lakini Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amekataa wazo la kusitishwa kwa mapigano sasa ambalo litaiacha Urusi ikidhibiti karibu theluthi moja ya nchi yake na kutoa muda wa vikosi vyake kujipanga upya baada ya miezi 17 ya vita.

Rais Vladmir Putin aliahidi kuzingatia mahitaji ya nafaka ya Afrika / picha: Reuters 

Katika mkutano huo, Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi aliitaka Urusi kufufua mkataba wa nafaka wa Bahari Nyeusi ambao Moscow ilikataa kuufanya upya wiki iliyopita.

Ulikuwa umeipa Ukraine "ukanda salama" wa kusafirisha nafaka kutoka bandari zake licha ya mzozo huo.

Misri ni mnunuzi mkubwa wa nafaka kupitia njia ya Bahari Nyeusi, na rais Sisi aliuambia mkutano huo "ni muhimu kufikia makubaliano" juu ya kufufua mpango huo.

TRT Afrika na mashirika ya habari