Ramadhan Kibuga
TRT, Afrika, Bujumbura, Burundi
Wakati kuhesabiwa kwa kura zilizopigwa Disemba 20 na 21 kukiendelea nchini DRC, mapigano yameibuka upya siku ya Ijumaa katika eneo la Masisi mashariki mwa DRC. Waasi wa M23 wanakabiliana na wanamgambo watiifu kwa serikali wakishirikiana na jeshi la Congo. Hayo yanajiri licha ya usitishwaji wa mapigano wa wiki mbili uliotangazwa tarehe11 Disemba.
Usitishwaji wa muda wa mapigano ulitangazwa na Marekani na kuthibitishwa siku kadhaa baadae na pande mbili husika: waasi wa M23 na viongozi wa Congo.
Baada ya siku 10 za utulivu, mapigano yamerudi upya katika eneo la Masisi kuanzia siku ya Alhamisi na kuendelea Ijumaa katika vijiji vya Kibarizo na Matanda. Taarifa hizo za mapigano zimethibitishwa pia na mashirika ya kiraia.
Téléphore Mitondeke wa Shirika la Kiraia alifichua kwamba " hali ya usalama inazidi kudorora siku hadi siku kwa sababu wakazi wametoroka nyumba zao. Sio tu wamekosa haki yao ya msingi ya kura lakini pia wanayakimbia makazi yao kutokana na vita''
Raia wakazi wa vijiji mbalimbali vya maeneo ya Rutshuru, Masisi na Kwamouth hawakupata haki ya kupiga kura kutokana na usalama mdogo kwenye maeneo hayo ambayo sehemu kubwa yako mikononi mwa waasi wa M23. Waasi hao wanadaiwa kuungwa mkono na Rwanda kwa mujibu wa ripoti za wataalamu huru wa Umoja wa Mataifa. Hata hivyo, mara zote, Rwanda imekuwa ikikanusha tuhuma hizo.
Siku mbili kabla ya usitishwaji mapigano, mgogoro huo ulishuhudia jeshi la Congo likishambulia ngome za kikundi cha M23 kwa kutumia ndege za kivita.
Hayo yakiarifiwa, uhesabiaji wa kura umeanza Ijumaa hii usiku katika Kituo cha kukusanya matokeo mjini Kinshassa cha 'Bosolo.'
Uchaguzi huo uligubikwa na dosari nyingi za kiufundi na uhaba wa vifaa kwa mujibu wa ripoti za awali za timu mbali za waangalizi wa kitaifa na kimataifa.
Lakini Mkuu wa Tume Huru ya Uchaguzi CENI Denis Kadima amejipongeza kwa hatua hiyo, ''Nimesikia baadhi ya watu wanasema uchaguzi huu ulikuwa mbovu na wa balaa. Sisi tunachukulia kama muda haukuwa rafiki kwetu. Lakini tulipambana kwa hali zote. Lengo letu halikuwa kutaka kusifiwa. Lakini lengo letu ni kuruhusu Wakongomani kushiriki katika mchakato wa wazi, wa ushindani, wa demokrasia na wa haki. Kama kuna watu wanaona tumefeli sisi tunaona tumefaulu.''
Matokeo yanatarajiwa kuendelea yanatolewa lengo ikiwa ni kumpata mshindi wa urais kabla ya mwaka kumalizika.