Na Takunda Mandura
Aluwaine Tanaka Manyonga alisomea uhandisi wa umeme katika kipindi ambacho Zimbabwe ilikuwa inapitia mgao mkubwa wa nishati ya umeme.
"Ilifika wakati tunakosa umeme kwa saa zipatazo 19 kwa siku," anaiambia TRT Afrika.
"Nilidhani kuwa suluhu niliyokuwa naifanyia majaribio kwa tatizo la umeme lingenipotezea muda wangu wa masomo."
Hata hivyo, ikiwa imeanza kama utundu wa kuchokonoa vifaa vya umeme, uvumbuzi wa Manyonga sasa unastawisha ndoto na malengo ya watoto wengi waishio kwenye maeneo yasiyojua umeme.
Kupitia ugunduzi wake, aliouita Chemli ya Chigubhu, Munyonga sasa anawawezesha wanafunzi wa shule kujisomea nyakati za usiku.
Kifaa hicho, ambacho ni rahisi kubeba kimetengezwa kwa kutumia taka ngumu.
Uwezo wa kifaa hiki umejizolea sifa kutoka kwa watu wanaounga mkono matumizi ya teknolojia yenye kuhifadhi mazingira, haswa haswa kupitia uundwaji na upatikanaji wake.
Kuondoa giza
Kulingana na ripoti ya benki ya dunia ya mwaka 2021, inayohusu maendeleo ya matumizi ya nishati duniani, chini ya asilimia 50 ya wananchi wa Zimbabwe wanapata huduma ya umeme. Hali ni mbaya zaidi kwa maeneo ya vijijini, kwani ni asilimia 30 tu ndio wanapata nishati hiyo.
Changamoto ya umeme nchini Zimbabwe imekuwa na madhara makubwa sana kwenye sekta ya elimu.
Manyonga, mhitimu kutoka Chuo Kikuu cha Zimbabwe, aliunda taa ya Chigubhu, wakati akijaribu kuua ndege wawili kwa jiwe moja.
Baada ya kushawishika na uendelevu wa teknolojia hiyo, Manyonga aliamua kusajili kampuni yake mwenyewe kwa jina la Zambezi Ark Technology (Zar Tech) mwaka 2022, ili imrahisishie kupeleka huduma kwa watu.
Kwa kiasi kikubwa, Zar Tech imewezesha jamii nyingi za vijijini nchini Zimbabwe kubadilisha maisha yao, toka kuanzishwa kwake.
Teknolojia hiyo, iliyo rafiki kwa mazingira imewezesha kupunguza uchafuzi wa mazingira kwa kurudia matumizi ya vifaa vya umeme vilivyotumika na kutupwa kama takataka.
"Niliumiza kichwa sana kutafuta kasha sahihi wakati naandaa ugunduzi huu, lakini baadaye nikagundua kumbe ninaweza kutumia taka ngumu zilizopo kwenye madampo, hakika inatia moyo kuona kifaa hiki kikifanya kazi kwa ustadi mkubwa sana," Manyonga anasema.
Faida nyingi
Kaya nyingi nchini Zimbabwe zinatumia vifaa vya umeme vilivyotengenezwa China. Hata hivyo, kiasi kikubwa cha vifaa hivyo ni duni na visivyodumu.
"Mbali na hitaji la kutafuta njia mbadala ya umeme wa kawaida, moja ya mambo yaliyonifanya nianzishe mradi huu ni kutokuwa na uhakika wa taa za kudumu. Taa nyingi za LED hazidumu kwa muda mrefu na hutupwa kwenye madampo, na hivyo kuongeza mzigo wa takataka," anafafanua Manyonga.
Wakati dunia inapambana na changomoto ya uwepo wa taka ngumu, nchi ya Zimbabwe huzalisha takribani tani milioni 1.9 za takataka kila mwaka, sawa na asilimia 20 ya taka zote zinazozalishwa nchini humo.
Wataalamu wana amini kwamba ugunduzi tofauti, hasa ulio rafiki kwa mazingira una uwezo wa kuwa muarobaini wa kudumu wa uwepo wa taka ngumu.
Sifa na Msukumo
Mnyonga ni mtu mwenye furaha kuona wanafunzi, hasa wale wanaotokea maeneo ya vijijini wakifaidika na ugunduzi wake.
Hadi kufikia sasa, wanafunzi wa shule mbili katika kijiji cha Chihota, wamepokea mafunzo ya awali ya namna ya kutengeneza vyanzo endelevu wa umeme. Hali kadhalika, kiwanda cha Zar Tech kimeazimia kufikia watoto 6,000, hadi kufikia mwisho wa mwaka 2024.
"Nadhani tuna uwezo wa kuwafikia wanafunzi wengi zaidi kwani kazi yetu inaungwa mkono na mashirika tofauti," anasema Manyonga.
Manyonga ameshinda tuzo kadhaa kupitia ugunduzi wake, ikiwemo ile aliyopewa nchini Misri kwenye mkutano wa mkutano wa 27 wa nchi wanachama wa mkataba wa Kimataifa wa tabianchi (COP 27).