TANESCO imesema kuwa hatua hiyo itachangia upatikanaji wa umeme kwa njia bora katika maeneo zaidi nchini humo./ Picha :   TANESCO

Katizo la umeme kwenye baadhi ya maeneo nchini Tanzania iliyoanza wiki hii inatarajiwa kuendelea huku Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) likiwataarifu wateja wake kuwa huduma hiyo ya umeme itakosekana kuanzia saa moja kamili asubuhi hadi saa kumi na mbili jioni (01:00 -12:00) kuanzia tarehe 26 hadi 28 Agosti 2023.

Sababu ya kuzimwa kwa umeme

Shirika la usambazajia umeme TANESCO lenye makao makuu Dodoma, limefafanua kuwa umeme utazimwa kwa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa Kilovoti 220 kutokea Kidatu kwenda Kihansi ili kumwezesha mkandarasi kuunganisha njia mpya ya umeme kwenye gridi ya taifa.

Sababu ya kuzimwa kwa njia hiyo ni kuruhusu Mkandarasi anayejenga kituo kipya cha kupoza umeme Ifakara kuunganisha kituo hicho kwenye gridi ya taifa. Kazi hiyo itahusisha kuunga njia ya msongo wa Kilovoti 220 Kihansi-Kidatu kwenye kituo kipya.

TANESCO

Umuhimu wake

Aidha, TANESCO imeongeza kuwa hatua hiyo itachangia upatikanaji wa umeme kwa njia bora katika maeneo zaidi nchini humo.

"Kuunganishwa kwa kituo hiki kipya ni muhimu kwani kutasaidia kuongeza Ubora na upatikanaji wa umeme katika wilaya za Kilombero, Ulanga na maeneo ya jirani sambamba na kuvutia wawekezaji."

Maeneo yatakayoathirika

Shirika la TANESO lenye makao yake makuu jijini Dodoma, limeongeza kuwa shughuli hiyo italemaza upatikanaji wa huduma hiyo muhimu kwa vipindi tofauti haswa katika baadhi ya maeneo huku ikiahidi kuwafahamisha wateja wake pindi tu zoezo litakapokamilika.

Mikoa iliyotajwa na TANESCO ni Iringa Njombe, Ruvuma,Mbeya, Songwe, Dodoma, Singida Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Shinyanga, Simiyu, Tabora, Mwanza, Geita na Mara.

TRT Afrika