Kiwanda cha kuzalisha umeme kwa njia ya maji nchini Gabon. Picha / Reuters

Na

Firmain Eric Mbadinga

Umeme wenye thamani ya mamilioni ya dola, unaweza kuwa hata zaidi, uliuzwa kwa watumiaji nchini Gabon na walaghai ambao walianzisha mfumo sambamba wa malipo katika kampuni ya shirika la umeme inayoendeshwa na serikali, uchunguzi wa mamlaka umebaini.

Kiwango cha hasara katika Société d'énergie et d'eau du Gabon (SEEG) bado kinatathminiwa, lakini washukiwa waliweza kuzalisha na kuuza tikiti za umeme bila hata senti moja kwenda kwa kampuni hiyo.

Maelezo ya ubadhirifu huo yalifichuliwa mwezi huu kufuatia uchunguzi wa ndani, maafisa wa kampuni hiyo walisema.

Uchunguzi ulibaini mpango huo ulikuwa kazi ya ndani, na kusababisha kukamatwa kwa wafanyikazi kadhaa ambao wamehojiwa na 'Direction Générale des Recherches (DGR)'.

Matatizo ya kifedha

Meneja Mkuu wa SEEG, Joël Lehman Sandoungout, amekiri kuwepo kwa ubadhirifu huo ambao alisema umekuja wakati kampuni hiyo tayari inakabiliwa na matatizo ya kifedha.

"Uchunguzi unaendelea. Tuna mawakala (wafanyakazi) ambao wanahojiwa katika DGR,'' Sandoungout alithibitisha kwa TRT Afrika.

Wakili anayewakilisha kampuni hiyo alisema hasara za kifedha zilikuwa "kubwa". "Walionufaika na ulaghai huu, ambao walikuwa wamejificha kwenye vivuli, wanaanza kujitokeza, na kufanya operesheni kuwa nyeti," Anges Kevin Nzighou, mshauri wa sheria wa SEEG, aliiambia TRT Afrika.

Ulaghai ulichukua muda gani

Bado haijafahamika ni muda gani operesheni hiyo ilifanyika lakini kuna tuhuma kuwa inaweza kuwa kwa miaka mingi. Wagabaon wengi nchini wanaufananisha na msemo maarufu wa Gabon: Siku elfu kwa mwizi na siku moja kwa mmiliki.

Watumiaji wa umeme nchini wanapaswa kununua tokeni za kulipia kabla kutoka kwa msambazaji wa umeme ili kuweka nambari ambayo huwekwa kwenye mita zao na kuhakikisha kupatikana wa umeme.

Umeme unaotolewa kwa wateja unategemea tokeni iliyonunuliwa. Washukiwa hao walifanikiwa kuuza tokeni hizo za umeme bila kuhamisha mapato kwa SEEG, kulingana na uchunguzi.

Ulaghai wa seva

Ukaguzi wa ndani uliibua tuhuma za ulaghai kwenye seva na kusababisha uchunguzi zaidi wa kampuni. Washiriki wanaoshukiwa ni wakuu wawili wa kitengo na meneja wa IT.

Washukiwa hao bado hawajafunguliwa mashtaka mahakamani na hawajazungumza hadharani kuhusu tuhuma hizo.

Mamlaka imefanya upekuzi katika eneo la mtoa huduma mkuu, Sigma Technologie, ambako mfumo huo sambamba inasemekana umewekwa.

Sigma Technologie haijatoa maoni hadharani kuhusu uchunguzi huo.

''Mnamo Agosti 09, 2024, SEEG iliwasilisha malalamiko mawili ya wizi na ubadhirifu. Uchunguzi unaoendelea unafichua vijezi vipya kila siku, na kufichua ukubwa wa ulaghai huu mkubwa," msambazaji wa nguvu alisema.

Kuboresha mifumo

SEEG tayari imetangaza kuwa itakuwa ikiboresha mifumo yake ya usalama ya IT ili kuimarisha ufuatiliaji na kugundua majaribio yoyote ya kuendesha mifumo na data zake.

Ukaguzi huru wa mifumo ya usimamizi wa tikiti za mauzo ya umeme pia utafanywa, ilisema. Wakati huo huo, pamoja na hatua za kisheria, kampuni imeanzisha mapitio ya mikataba na washirika wa nje ili kuimarisha usalama wa uendeshaji.

TRT Afrika