Takriban manusura 50 wa ajali ya boti ya wahamiaji ya mwezi uliopita iliyosababisha vifo vya watu 25 katika Bahari ya Hindi karibu na Madagascar wamerudi nchini Somalia Jumamosi na kupokelewa na maafisa wa serikali.
Manusura wa umri wa miaka 17 hadi 50 walivalia mavazi yaliyotengenezwa kwa vitambaa vyenye rangi ya bendera ya taifa la Somalia walipokuwa wakishuka kutoka kwenye ndege katika mji mkuu, Mogadishu, wakionekana kufarijika kurudi salama.
Vijana wengi wa Kisomali hujiingiza kila mwaka katika safari za hatari kwa ajili ya kutafuta fursa bora nje ya nchi.
Shirika la Umoja wa Mataifa hapo awali liliibua wasiwasi juu ya kuongezeka kwa uhamiaji usio wa kawaida kutoka nchi za Pembe ya Afrika huku watu wakikimbia migogoro na ukame.
Watu walionusurika waliliambia Shirika la Habari la The Associated Press kwamba raia hao walikwama baharini kwa muda wa siku 13 baada ya injini za boti yao kuharibika.
Ahmed Hussein, ambaye alikuwa akisafiri na binamu yake ambaye sasa ni marehemu, alisema walikuwa wakielekea Ulaya wakiwa na matumaini ya maisha bora.
Meli mbili zilizowabeba wahamiaji hao ziliondoka Somalia mapema mwezi uliopita.
"Tuligawanywa katika mashua mbili ndogo. Injini iliharibika, nasi tukaelea baharini kwa siku 13 bila injini inayofanya kazi. Hatukuwa na chakula wala maji. Tulinusurika kwa kuvua samaki,” alisema.
Maafisa wa Madagascar na Somalia walisema awali boti hizo zilipinduka lakini hawakutoa maelezo zaidi.
Mamlaka pia ilikuwa imeweka idadi ya walionusurika kuwa 48, lakini ni 47 pekee waliofika Somalia, na hakuna maelezo zaidi kuhusu mtu mmoja aliyenusurika.