Takriban raia mia nne wa Nigeria waliohamishwa kutoka Sudan wamewasili nyumbani baada ya siku nyingi za safari ngumu ya barabara na anga.
Walikuwa kundi la kwanza la Wanigeria kurejeshwa makwao huku uhamisho mkubwa wa wageni kutoka Sudan ukiendelea kutokana na mapigano yanayoendelea katika nchi hiyo ya Afrika Kaskazini.
Tume ya Raia wa Nigeria Diaspora, wakala wa serikali unaosimamia masuala ya Wanigeria wanaoishi nje ya nchi, walisema takriban ''wahamishwaji 376'' waliwasili katika mji mkuu wa Abuja Jumatano usiku.
Wengi wa waliohamishwa walionekana kuchoka walipowasili lakini walisema walikuwa na furaha kurejea nyumbani baada ya kutoroka ghasia nchini Sudan.
Walisafirishwa kwa ndege ya kijeshi na ndege ya kibiashara kutoka mji wa Aswan Misri kwa safari ya saa tano baada ya kusafiri katika msafara wa mabasi 13 kutoka mji mkuu wa Sudan Khartoum na kukwama kwa siku kadhaa kwenye mpaka wa Misri kutokana na masuala ya visa.
Mamlaka ya Misri ilikuwa imewanyima Wanigeria ruhusa ya kuvuka mpaka walipoondoka Sudan Alhamisi wiki iliyopita lakini Jumatatu ilikubali kuwaruhusu kuvuka baada ya Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari kuingilia kati, kulingana na Tume ya Wanigeria katika Diaspora.
Mabasi mengine 20 yaliyotayarishwa kuwahamisha mamia ya raia wa Nigeria yanaripotiwa kuwa bado yako Sudan.
Msafara huo hautasafiri tena kwenda Misri, lakini hadi Port Sudan, mji ulio kwenye Bahari Nyekundu kilomita 675 (maili 420) kutoka Khartoum, kutoka hapo wangesafiri kurejea Nigeria, msemaji wa Shirika la Kitaifa la Usimamizi wa Dharura aliiambia AFP.
Kulingana na mamlaka ya Nigeria, mpango wa uokoaji unahusisha zaidi ya raia 3,500, lakini idadi yao inaweza kuwa kubwa zaidi.
Maelfu ya Wanigeria wanaishi Sudan, wengi wao wakiwa wanafunzi na wafanyabiashara.
Mapigano nchini Sudan yamesababisha vifo vya takriban watu 550, maelfu ya watu kuyahama makazi yao na kusababisha kuhama kwa wageni.
Pande zinazopigana - jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa haraka vilikubaliana juu ya usitishaji vita wa siku saba kuanzia Jumatano huku shinikizo la kimataifa la kukomesha umwagaji damu likiongezeka.
Pande hizo mbili ambazo zilikuwa washirika zimekuwa zikipigania udhibiti wa nchi tangu mwezi uliopita baada ya wiki kadhaa za kutokubaliana juu ya mpango wa mpito kwa utawala wa kiraia huku kuunganishwa kwa Vikosi vya Msaada wa Haraka vya kijeshi katika jeshi la kawaida likiwa suala kuu linaloshikilia.