Conference on Human Capital

Viongozi wa Afrika wametakiwa wawekeze zaidi katika vijana hasa wanawake ili kujenga nguvu kazi ya siku zijazo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Mh Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwa jukumu lipo kwa viongozi hao kuweka mustakbali safi wa ukuaji wa uchumi wa Afrika kwa kuwekeza kwa ujasiri.

''Ni muhimu sisi kama viongozi tuhakikishe kwamba tunaleta mageuzi yote muhimu kuliwezesha bara hili litumie uwezo na rasli mali zake kujikomboa kiuchumi,'' amesema mama Samia akihutubia kongamano jijini Dar es Salaam.

Inakisiwa kuwa kufikia 2050, Afrika itatoa mataifa 10 yenye idadi kubwa zaidi ya vijana duniani. Picha TRT Afrika

Zaidi ya wajumbe 2000 wakiwemo viongozi wa nchi, mawaziri, wadau wa uchumi na maendeleo, mashirika yasiyo ya serikali na vijana wajasiria mali wamehudhuria kongamano hilo lililoandaliwa na Tanzania kwa hisani ya Benki ya Dunia.

''Viongozi wamezungumzia umuhimu wa kuongeza idadi ya ajira na kuwawezesha vijana kupata taaluma za kujikimu kiuchumi,'' anasema Philomen Henry Maluka, kijana mjasiria mali anayehudhuria kongamano hilo.

''Lakini pia wale vijana wanaojiajiri wenyewe na wenye ubunifu mbali mbali wanawezeshwa katika kutanuliwa masoko yao ili waweze kuonyesha bunifu zao mbalimbali.'' ameongeza Maluka.

Kauli mbiu ya kongamano hilo ni 'Kuongeza uzalishaji wa vijana kupitia mafunzo na ujuzi.' Picha : Ikulu TZ

Inakisiwa kuwa kufikia 2050, Afrika itatoa mataifa 10 yenye idadi kubwa zaidi ya vijana duniani.

''Habari hii ni nzuri na mbaya vile vile kwetu,'' anasema Mh. Rais Samia Suluhu.

''Hali hii inaweza kuwa nzuri na yenye tija iwapo tutawekeza kwenye raslimali watu kwa kuhakikisha uwepo wa afya bora, elimu bora yenye stadi za maisha ili kujenga nguvu kazi yenye tija kama ilivyo kwa wenzetu wa Asia.'' Anaongezea Rais Samia. ''Hatma inaweza kuwa mbaya iwapo hatutafanya uwekezaji sahihi.''

Kauli mbiu ya kongamano hilo ni 'Kuongeza uzalishaji wa vijana kupitia mafunzo na ujuzi.'

Zaidi ya wajumbe 2000 wakiwemo viongozi wa nchi, mawaziri, wadau wa uchumi na maendeleo, Pich : Ikulu TZ

Hii inaendana na maono ya bara kama walivyosema viongozi mbali mbali katika mkutano huo akiwemo mkuu wa Benki ya Dunia.

''Thuluthi moja ya tofauti zinazoibuka kati ya nchi tajiri na maskini zinatokana na uwepo au upungufu wa raslimali watu,'' amesema makamu wa rais wa maendeleo ya rasilimali watu katika Benki ya Dunia Mamta Murthi.

Bi Murthi alipongeza mataifa ya Afrika katika hatua walizopiga katika kutoa elimu kwa vijana kuanzia kiwango cha chini zaidi hadi vyuo.

Hata hivyo ametahadharisha viongozi kuzingatia viwango vya elimu vinavyotolewa.

Viongozi mbalimbali kutoka ndani na Nje ya Tanzania wakiwa kwenye ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC) kwa ajili ya kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Rasilimali Watu / Picha: Ikulu TZ

''Viwango vya masomo vinatakiwa kuendana na mahitaji ya nguvu kazi ya kila nchi,'' aliongeza Murthi. ''Lazima kuwe na ushirikiano katika kuwapa vijana elimu inayokuza upamoja katika kazi, fikra za kuuliza, na jitihada za kazi.'' Aliongeza.

Miongoni mwa mataifa yaliyotajwa kuwa na sera bora za elimu zinazoweza kuigwa ni pamoja na Rwanda, Kenya, Nigeria na Msumbiji. Tanzania imesifiwa hasa kwa sera ya kuwarudisha wasichana waliojifungua shuleni kuendelea na masomo yao.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu UNFPA, Bara Afrika lina idadi kubwa zaidi ya vijana duniani, huku zaidi ya 70% ya watu wake wakiwa chini ya umri wa miaka 30. Idadi hiyo kubwa ya vijana ni fursa kwa ukuaji wa bara - lakini iwapo tu vizazi hivi vipya vitawezeshwa kikamilifu kutambua uwezo wao kamili.

TRT Afrika