Waombolezaji kutoka Malawi na wageni wengine wa kimataifa walihudhuria mazishi ya Makamu wa Rais Dk. Saulos Chilima huko Ntcheu, nchini Malawi, siku ya Jumatatu.
Umati wa watu ulikusanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi ya Nsipe huko Ntcheu kushuhudia Chilima, ambaye alifariki katika ajali ya ndege Jumatatu, Juni 11, 2024, akipumzishwa.
Katika hotuba ya rambirambi, mwakilishi wa familia ya marehemu, Elizabeth Mkandawire Mwanga, alisema makamu wa rais aliyefariki alikuwa “mtu mwenye furaha, upendo, na mkarimu, aliyekuwa na nafasi ya kuwa kiongozi wa kimataifa.”
“Niruhusuni nitoe shukrani kwa United Transformation Movement (UTM) kwa msaada waliotoa wakati wa maombolezo, na asante kwa machifu kwa upendo. Ningependa kuwashukuru watu wa Malawi kwa moyo wa upendo wakati wa maombolezo.
“Natoa wito kwa serikali kufanya uchunguzi ili kubaini ukweli na kuhakikisha kuwa janga kama hili halitokei tena. Niruhusu nitoe wito kwa taifa kuendeleza ndoto ya Chilima na kutokata tamaa ili ndoto zake ziweze kutimia,” alisema Mwanga.
Uchunguzi waamrishwa
Rais Chakwera, wakati wa hafla ya mazishi ya marehemu Chilima huko Bing Stadium, Lilongwe Jumapili, alisema tayari amewaomba nchi nyingine kusaidia katika uchunguzi.
“Ninaelewa kuwa Jeshi la Ulinzi la Malawi (MDF) lina taratibu zake za kufanya uchunguzi; hata hivyo, hilo pekee halitoshi. Kwa hiyo, kwa sasa, ni muhimu kuhusisha wachunguzi huru ili kwamba Wamalawi wote, pamoja na mimi, tuwe na majibu thabiti juu ya kile kilichotokea kweli.
“Nawaomba Wamalawi wote kuwa watulivu na wenye subira, tunaposubiri matokeo ya uchunguzi. Pia nataka kuwahakikishia kwamba kila Mmalawi atajua matokeo ya uchunguzi mara utakapokamilika” alisema Chakwera.
Watu mashuhuri waliohudhuria mazishi ni pamoja na rais wa zamani Dk. Bakili Muluzi, rais wa zamani Peter Mutharika, makamu wa rais wa zamani Khumbo Kachali, na Katibu Mkuu wa UTM Patricial Kaliati, miongoni mwa wengine.
Wa kwanza kuweka mashada ya maua alikuwa mjane wa Chilima, Mary Chilima, kisha Rais Chakwera na mkewe, Monica Chakwera, kisha Rais wa zamani Peter Mutharika na mkewe, Gertrude Mutharika, miongoni mwa wengine.
Marehemu Chilima na wengine tisa walikufa katika ajali ya ndege katika Msitu wa Chikangawa katika wilaya ya Mzimba.