Na Coletta Wanjohi
TRT Afrika, Istanbul
Raia wa Sudan walipoukaribisha mwaka wa 2023, hawakujua kuwa nchi yao ingekumbwa na migogoro ndani ya miezi minne tu tangu kuanza kwa mwaka huu.
Pande mbili ambazo ndizo awali zilizoshirikiana mwaka 2019 kumtimua aliyekuwa madarakani wa rais wa nchi hiyo Omar el Bashir zilianza kuzozana mwezi Aprili mwaka huu.
Mapigano yaliibuka tarehe 15 Aprili kati ya vikosi vya Jeshi la Sudan vinavyoongozwa na Jenerali Al Burhan na Vikosi vya Rapid Support Forces vinavyoongozwa na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo.
Mgogoro huu, uliondoa matumaini ya watu wa Sudan ya kuanza kwa mchakato wa kuwepo kwa serikali ya kidemokrasia itakayoongozwa na raia. Mkataba wa Desemba 2022 kati ya wanajeshi nchini Sudan na vyama vya siasa ulikuwa umetoa kipindi cha miaka miwili kuelekea uchaguzi.
Maafa ya kibinadamu yanaendelea kulikumba taifa hilo, ambalo ni la tatu kwa ukubwa barani Afrika likiwa na idadai ya zaidi ya watu milioni 48.
Hivi sasa, nusu yao watahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu kufikia mwaka 2024, kutokana na mzozo unaoendelea, hayo ni kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.
Kufikia Disemba 2023 Umoja wa Mataifa unasema watu milioni saba wameripotiwa kuyaacha makazi yao ndani na nje ya nchi.
Wimbi hili la wakimbizi, limebebesha mzigo mkubwa nchi jirani kama vile Chad, Misri na Sudan Kusini.
"Wakimbizi milioni saba wamekimbia makazi yao, na ulimwengu umebaki kimya," Filippo Grandi, Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi, UNHCR anasema.
Zaidi ya watu 12,000 wameripotiwa kuuawa katika mzozo huo kulingana na Shirika linalokusanya taarifa za migogoro la Armed Conflict Location & Event Data Project (ACLED).
Kati ya hao, 20 walikuwa ni wafanyakazi wa misaada na wengine 36 wamejeruhiwa.
Hata hivyo, licha ya kuibuka kwa janga hilo la kibinadamu, na kuwepo kwa jitihada za kujaribu kutuliza hali, lakini mahasimu hao wawili, bado hawajaamua kuweka silaha chini.
"Jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka vina silaha nyingi na nguvu nyingi za kijeshi na wanahisi wanatatua matatizo yao kwenye uwanja wa vita," Dkt. Edward Githua, mtaalam wa mahusiano ya kimataifa anaiambia TRT Afrika.
Wakati mzozo ukiendelea ndivyo uhaba wa chakula unavyoongezeka huku mamilioni ya watu wakishindwa kujihusisha na uzalishaji wa kilimo.
"Watu milioni 17.7 kote nchini Sudan, ambayo ni asilimia 37 ya watu waliochunguzwa, watakabiliwa na viwango vya juu vya uhaba wa chakula, kati ya Oktoba 2023 na Februari 2024." WFP inaieleza Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa FAO katika ripoti yake iliyoitoa Disemba, 2023.
"Idadi kubwa zaidi ya watu walio na uhaba wa chakula iko katika majimbo yaliyoathiriwa na viwango vya juu vya ghasia zilizopangwa, ikiwa ni pamoja na Darfur Kuu, Greater Kordofan na Khartoum - hasa katika eneo la miji mitatu la Khartoum, Bahri na Omdurman."
Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula pia limesema katika tathmini yake ya hivi karibuni kwamba uporaji mkubwa wa masoko, benki, viwanda na majengo ya umma umesababisha kuongezeka kwa uhaba wa huduma muhimu, chakula na bidhaa zisizo za chakula kote nchini, na kuzidisha hali mbaya ya uhaba wa chakula na hali ya utapiamlo.
Je, amani itakuja lini nchini Sudan?
Umoja wa Afrika (AU) umesisitiza kuwa suluhu inayoongozwa na Sudan ndiyo njia pekee ya nchi hiyo kujitoa katika vita vinavyoendelea hivi sasa.
Katika Mkutano wa 41 wa Mamlaka ya Serikali ya Maendeleo, IGAD ambayo Sudan ni mwanachama, msisitizo ulikuwa haja ya kuwepo kwa "mchakato wa upatanishi uliounganishwa na Afrika." Mkutano huo ulifanyika Djibouti tarehe 9 Desemba, 2023.
Katika mkutano huo, pande zote mbili zinazozozana, ziliahidi mbele ya viongozi wa kikanda kuwa zitafanya maongezi.
Viongozi wa eneo hilo walisema katika taarifa waliyoitoa baada ya mkutano kuwa, Jenerali Abdel Fattah Al-Burhan "ametoa ahadi ya kusitisha vita bila masharti na utatuzi wa mzozo kupitia mazungumzo ya kisiasa na kuwa na mkutano wa moja kwa moja na Kamanda wa Kikosi cha Rapid Support Forces (RSF) kutokana na muongozo wa IGAD."
IGAD pia ilithibitisha kwamba kupitia mazungumzo ya simu na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo wa RSF ambaye alikubali pendekezo la "kusitishwa kwa mapigano bila masharti, utatuzi wa mzozo kupitia mazungumzo ya kisiasa na kufanyika kwa mkutano kwa mujibu wa muongozo wa IGAD."
Uamuzi wa IGAD sasa ni kuharakisha mazungumzo yanayohusisha Wasudan yanayoongozwa na Sudan ambayo yatapelekea kuundwa kwa serikali ya mpito inayoongozwa na raia na baadaye kufanyika kwa uchaguzi wa kidemokrasia.
Lakini je, majenerali wataheshimu ahadi hizi?
Hii sio mara yao ya kwanza kuhimizwa kukaa mezani kujadili amani ya nchi yao.
Mazungumzo ya Jeddah kama yalivyoitwa, yaliyowezeshwa na serikali ya Marekani na Saudi Arabia hayajazaa matokeo yoyote ya kudumu.
Mazungumzo hayo yalianza mwezi Mei 2023, yakasitishwa Juni na kuanza tena Oktoba huku pande zinazopigana zikiahidi kuruhusu ufikaji wa misaada ya kibinadamu na kuimarisha njia za mawasiliano.
Mwezi Disemba 2023 mazungumzo hayo yalisitishwa bila mafanikio yoyote.
"Jambo moja ambalo liko wazi ni kwamba watu wa Sudan wanataka mabadiliko na maisha yao yaendelee kuelekea utawala wa kiraia," mjumbe wa zamani wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen, Jamal Benomar ameiambia TRT Afrika.
"Tusiamshe Darfur"
Huku bara la Afrika likingoja utimizaji wa makubaliano ya hivi majuzi kati ya majenerali ya kurudisha hali ya kawaida nchini Sudan, wasiwasi uko katika eneo la Darfur ambapo machafuko yamefika.
Mji mkuu wa Sudan Khartoum ndio uwanja mkuu wa vita kwa majenerali hao wawili, mapigano yalipoanza mwezi Aprili 2023 yalienea katika eneo la Darfur kulingana na takwimu za Shirika linalokusanya taarifa za migogoro, ACLED, ukosefu wa usalama unaongezeka katika eneo la Darfur.
Mzozo huku Darfur ulizuka tangu Aprili 2003 wakati wengi wao wasio Waarabu walichukua silaha dhidi ya serikali, wakilalamikia ubaguzi na ukosefu wa maendeleo.
Kwa upande wake, serikali ya Sudan wakati huo ilikusanya wanamgambo wengi wa kiarabu, waliojulikana kama Janjaweed, kupigana na waasi.
"Changamoto kubwa ni kwamba vita hivi sasa vinaiamsha Darfur," Davd Matsanga mchambuzi wa masuala ya kisiasa anaieleza TRT Afrika," kama hatutakuwa makini vita hivi vitazua tena machafuko zaidi huko Darfur na basi mgogoro huu utakuwa na uharibifu mkubwa sana,” anasema.
Kulingana na ACLED, ukosefu wa usalama tayari unaongezeka katika eneo la Darfur.
"RSF inahamia kwa mamlaka inayotawala huko Darfur, huku kiongozi wa RSF Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana kama Hemedti, akihimiza jumuiya za mitaa kuunda mamalaka zao wenyewe na kujitawala," uchambuzi wake wa hivi karibuni wa mzozo wa Sudan unasema.
Amani Africa, ACLED , inaendelea kuonya kwamba, ikiwa vita nchini Sudan havitakomeshwa, basi vitafungua matatizo makubwa ya ukosefu wa amani na usalama barani.
"Miongoni mwa mambo mengine, ni kutoa uwezekano wa kuvutia vikundi vya kigaidi na kuibuka kwa uhalifu kama vile mzunguko haramu na biashara ya silaha, unyonyaji haramu wa maliasili na uchumi wa vita kwa ujumla," ilisema katika taarifa.
Wataalamu wamevitaja vita vya Sudan kama vita vya kiburi vilivyojaa ubinafsi na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 12,190 tangu mapigano hayo yalipoanza katikati mwa mwezi wa Aprili.
Wanasema mzozo huo hauwezi kuwa na sura ya kibinadamu zaidi ya watu milioni saba waliolazimika kutafuta mahali pa kukimbilia kwa sababu eneo waliloliita nyumbani sio mahali salama tena.
Macho yote sasa yanaelekezwa kwa Jenerali Al Burhan na Jenerali Dagalo kuona kama mwaka 2024 utaleta hali ya kawaida inayohitajika baada ya ahadi yao ya kufanya maafikiano ambayo walitoa katika mkutano wa marais wa IGAD Disemba 2023.