Katika Afrika Mashariki, hali ya hewa ya El Niño ilileta mvua kubwa kuanzia mwezi Machi hadi Mei, na kusababisha mafuriko katika nchi kama Kenya, Tanzania, Somalia na Rwanda. /Picha: Wengine

Na Dayo Yusuf

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Katika mwaka wa 2024, Afrika ilikabiliwa na mfululizo wa majanga makubwa ya asili, na athari kubwa katika maisha, uhai na uharibifu wa miundombinu katika bara zima. Mwaka huu umekuwa na matukio mabaya ya hali ya hewa yaliyochangiwa na mabadiliko ya tabia nchi, ikiwa ni pamoja na mafuriko makubwa, vimbunga na ukame.

Kwa bahati mbaya, kile ambacho kinaonekana kuzua wasiwasi mkubwa ni kuvurugika kwa misimu ya mvua na kiangazi, na pia kuongezeka kwa ukali wake.

Katika Afrika Mashariki, hali ya hewa ya El Niño ilileta mvua kubwa kuanzia mwezi Machi hadi Mei, na kusababisha mafuriko makubwa katika nchi kama Kenya, Tanzania, Somalia na Rwanda.

Ripoti zinaonyesha kuwa zaidi ya watu milioni 1 walikimbia makazi yao kutokana na uharibifu mkubwa uliotokea katika nyumba, mazao na miundombinu kwa ujumla. Milipuko ya kipindupindu iliripotiwa kutokana na maji machafu.

Afrika Magharibi na Kati ilikumbwa na mafuriko makubwa zaidi, na kuathiri zaidi ya watu milioni 4.

Nchi kama Chad, Nigeria, na Niger zinaripotiwa kushuhudia idadi kubwa ya watu waliohama makazi yao, huku zaidi ya watu 500,000 wakipoteza makazi yao na miundombinu muhimu kama vile mabwawa, shule na vituo vya afya vikiharibiwa vibaya.

‘‘Maeneo kadhaa katika Sahel na Pembe ya Afrika yaliendelea kukabiliwa na ukame wa muda mrefu, na kuathiri uzalishaji wa kilimo na kuzorota kwa uhaba wa chakula. Mamilioni ya watu waliachwa bila kupata chakula cha kutosha, hasa nchini Ethiopia, Somalia, na Sudan’’ (UNICEF)

Utabiri wa hali ngumu

Ikilinganishwa na miaka ya nyuma, misimu imebadilika miezi yake, wakati mwengine inawahi au kuchelewa, kama ilivyoonekana kwa mvua, inachelewa au inakosa kabisa kwa muda mrefu. Au mvua inanyesha wakati ambao sio msimu wake na kusababisha maporomoko.

Tayari tunavyochapisha wakati huu, kati kati ya Disemba 2024, kuna tahadhari imetolewa na Kituo cha Afrika cha ufuatiliaji wa Hali ya Hewa kwa Maendeleo barani Afrika ACMAD kuwa Afrika Mashariki inakabiliwa na wakati mgumu kuingia mwanzoni mwa mwaka ujao 2025, kutokana na ukame unaotabiriwa.

‘‘🌧️ Hali ya hewa ya mvua kuliko kawaida inatarajiwa katika sehemu ya Kusini mwa Afrika ☀️Hali Kavu-kuliko-Kawaida zimetabiriwa kwa Afrika Mashariki,’’ ilisem ACMAD katika ukurasa wake wa X, Zamani twitter.

Taswira ya mvua na ukame barani Afrika kama inavyotabiriwa na shirika la ACMAD.

Kimbunga Hidaya

Mbali na mvua na ukame, Kimbunga Hidaya, mojawapo ya vikali zaidi kuikumba Afrika Mashariki, kiliikumba Tanzania mwezi Mei, na kusababisha mafuriko na maelfu ya watu kuyahama makazi yao. Ingawa vifo vilikuwa vichache, kimbunga hicho kiliangazia udhaifu katika miundombinu ya pwani ya Afrika Mashariki.

Bwawa kupasuka

Mwishoni mwa Aprili, bwawa lilipasuka katika eneo la Rift Valley Kenya na kuwaua zaidi ya watu 100, huku wengine wengi wakiachwa bila makwao kwa kusombwa makaazi yao. Hii ni baada ya mvua kubwa kunyesha eneo hilo na kupasua kingo za mito.

Bwawa lililoporomoka Kaskazini Mashariki mwa Nigeria lilisababisha mafuriko na kusababisha hadi watu 200,000 kuyahama makazi yao huko Maiduguri. Mabwawa mengine katika eneo hilo yalikuwa chini ya shinikizo kubwa kutokana na mvua kubwa.

Majanga ya kimazingira pia husababisha moto katika misitu.

Mioto ya misitu

Afrika Kusini ilikumbwa na mioto ya misitu ya msimu katika sehemu za Rasi ya Magharibi, ikichochewa na hali ya ukame na upepo mkali. Moto huu uliathiri mifumo ikolojia na jamii za wenyeji.

Japo mioto ya ain ahii sio kitu cha kawaida kwa Afrika, imekumba nchi nyingi za Ulaya, Marekani na hata Australia ambako imesababisha vifo kadhaa na kuharibu mali ya thamani kubwa.

Sasa hofu ni kuwa, mioto kama hii imeanza kuonekana katika maeneo ya Afrika na kunako endelea kubadilika hali ya anga, ndivyo matukio yanatarajiwa kukithiri.

Maporomoko ya Ardhi

Mwezi Disemba tu, siku chache zilizopita Uganda ilikumbwa na maporomoko mabaya ya ardhi yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 100, kwenye miteremko ya Mlima Elgon, volkano iliyotoweka kwenye mpaka na Kenya, takriban kilomita 300 (maili 190) Mashariki mwa mji mkuu, Kampala.

Watu wakiwa wamebeba mwili wa raia aliyeuawa kutoka eneo la maporomoko ya ardhi Bulambuli, Uganda Novemba 29, 2024.

Tangu Oktoba, mvua kubwa isiyo ya kawaida imesababisha mafuriko na maporomoko makubwa ya ardhi katika baadhi ya maeneo ya Uganda, ambapo Shirika la Msalaba Mwekundu la Uganda limelaumu mabadiliko ya hali ya hewa.

Maafa haya yanaangazia uwezekano wa bara hili kuathiriwa na hatari zinazohusiana na hali ya hewa na hitaji kubwa la hatua za kukabiliana na hali ya hewa.

TRT Afrika