Idadi ya vifo vinavyotokana na Kimbunga Chido nchini Msumbiji imeongezeka hadi 73, maafisa wa usimamizi wa majanga wametangaza Alhamisi.
Katika taarifa mpya, Luisa Meque, Mwenyekiti wa Taasisi ya Kitaifa ya Kudhibiti Hatari za Majanga nchini (INGD), amesema wakati tathmini ikiendelea ya kiwango cha uharibifu uliosababishwa na kimbunga hicho katika taifa hilo la Kusini mwa Afrika, miili zaidi inaendelea kutambuliwa.
"Hatuwezi kufahamu idadi kamili ya watu waliokufa kutokana na dhoruba," alisema. Meque alisema kuwa idadi ya waliojeruhiwa pia inaongezeka kila siku.
"Hali yetu ni ya kutisha. Tunahitaji msaada mkubwa ili kujua idadi kamili ya walioaga dunia, vyenginevyo, inakuwa vigumu sana kwetu kupata miili, kwa sababu baadhi yao wamezikwa baada ya kuangukiwa na majengo,” alisema.
"Kadiri dhoruba ilivyotulia, kuna uwezekano kwamba idadi ya vifo itaongezeka kwani bado tunatathmini kiwango cha uharibifu," Meque alisema.
Takriban watu milioni 2.5 wanaripotiwa kuathiriwa na kimbunga hicho, Meque alisema.
Kulingana na Louise Eagleton, Mwakilishi wa UNICEF nchini Msumbiji, takriban watoto 90,000 "wameathirika zaidi" na kimbunga hicho.
“Takriban katika jamii zote zilizoathiriwa, kuna ongezeko la idadi ya watoto walioathiriwa. Hawa ni watoto ambao wanahangaika kutafuta riziki na makazi. Watoto wanavumilia hali mbaya ya kimbunga. Hali ya sasa nchini ni ya kuhuzunisha,” Eagleton alisema.
Siku ya Jumatano, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ilitoa Dola milioni 4 katika kukabiliana na kimbunga hicho katika nchi jirani ya Malawi.
Kulingana na Idara ya Masuala ya Maafa na Usimamizi wa nchi hiyo (DoDMA), idadi ya vifo imefikia 13 na watu 45,000 katika wilaya tano za mkoa wa Kusini wamekosa makazi.