Wananchi wa Afrika Mashariki wameonyesha hisia tofauti kufuatia matokeo ya utafiti wa Shirika la Afrobarometer unaoonyesha viwango vya imani kwa vikosi vya polisi katika nchi mbalimbali barani Afrika.
Utafiti huo, umeonyesha eneo la Afrika kaskazini likiongoza kwa kuwa na asilimia 51, huku maeneo ya mashariki na magharibi yakigawana asilimia 50, wakati Afrika ya Kati ikiwa na kiwango cha chini kabisa cha asilimia 37.
Baadhi ya wasomaji wa TRT Afrika, walionekana kuhoji uhalali wa matokeo hayo, huku baadhi wakionekana kuyatilia mashaka. Wengi wa wananchi, walionekana kuguswa na nafasi ya Jeshi la Polisi la Tanzania ambalo linatajwa kuwa moja ya taasisi bora zaidi barani Afrika.
“Hizo takwimu zenu sio za kweli. Tanzania hata kabla siku ya maandamano haijafika mitaa yote inajaa maaskari na magari ya vita, washawasha na mabomu ya machozi. Yani kwetu sisi maandamano yakitangazwa na serikali inatangaza hali ya hatari,” ameandika James Mboneka.
Wakati huo huo, Eden Kingu nae kutoka Tanzania ameandika kwamba, Tanzania ndio ingetakiwa kuwa nafasi ya kwanza kabisa na sio ya mwisho, akiungwa mkono na Baraka Jothan ambae ameandika, “Hiyo nafasi ya mwisho wameionea, ilibidi iwe ya kwanza.”
Hata hivyo, Mohammed Hamisi alionekana kuwa na maoni tofauti akisema, “Sasa Tanzania na maandamao wapi na wapi. Raia wenyewe tu waoga huku askari wanatoka vitambi.”
Kwa upande wake, Ojengo Kennedy kutoka nchini Kenya, anasema kuwa bado hawajaona mabadiliko ya kiutendaji licha ya jina la kikosi cha polisi nchini humo kubadilishwa kutoka ‘Kenya Police Force’ na kuwa ‘National Police Service.’
Nae Chiki Kuruka, anasema hakubaliani na matokeo ya utafiti huo kwani Kenya ndio ilitakiwa kuwa nambari moja na kumalizia kusema, “hawa polisi wana ukatili.”
Matokeo ya utafiti huu yanakuja baada ya kushuhudiwa kwa miezi kadhaa ya maandamano ya Gen Z nchini Kenya yaliyopinga kile kilichoitwa ‘mswada tata wa fedha’ huku raia hao wakitaka mabadiliko ya utawala.
Ni katika kipindi hicho, ambapo wananchi walishuhudia nguvu kubwa ya polisi ikitumika dhidi ya wananchi waliokuwa wakiandamana, ambapo kwa mujibu wa baadhi ya vyombo vya habari nchini humo, waandamanaji kadhaa waliuawa, huku wengine wakijeruhiwa.
Kwa upande wa Tanzania, pia kumeshuhudiwa hali ya msuguano kati ya vikosi vya polisi na baadhi ya wananchi hasa kutoka kambi ya upinzani Chadema, ambapo miezi kadhaa iliyopita, baadhi ya viongozi wa chama hicho cha upinzani walikamatwa baada ya kutaka kufanya maandamano, na baadae kuachiliwa.
Ni kutokana na matukio hayo, ambapo baadhi wanaonyesha kutoyaamini matokeo ya utafiki wa Afrobarometer ambayo utafiti wake umefanywa kati ya mwaka 2021 na 2023 katika nchi 39 barani Afrika.