Abdirahman Mohamed Abdullahi, maarufu kama Irro, alishinda uchaguzi wa Rais wa Novemba 13 dhidi ya Rais aliyeko madarakani, Muse Bihi Abdi. / Picha: AFP  

Mahakama ya Katiba ya Somaliland imethibitisha uchaguzi wa Rais uliofanyika Novemba 13, ambao ulimpa ushindi Abdirahman Mohamed Abdullahi.

Siku ya Jumatano, timu ya majaji kumi wa Mahakama ya Katiba nchini humo, iliridhia kuwa uchaguzi wa Rais wa Novemba 13 ulikuwa wa huru na wa haki.

Abdirahman Mohamed Abdullahi, maarufu kama Irro, alishinda uchaguzi wa Rais wa Novemba 13 dhidi ya Rais aliyeko madarakani, Muse Bihi Abdi.

Irro, ambaye aligombea kupitia tiketi ya chama cha Waddani alipata kura 407,908 ambayo ni sawa na asilimia ya 64 ya kura zilizopigwa.

Idadi ya wapiga kura

Kwa upande wake, Bihi ambaye aligombea kupitia tiketi ya chama cha Kulmiye alipata kura 225,519 ambayo ni sawa na asilimia 35 ya kura zote, na kushika nafasi ya pili.

Mgombea mwingine, Faysal Ali Warabe kutoka chama cha UCID alivuna kura 4,699 ambazo ni sawa na asilimia 0.7 ya kura zote.

Kupitia matokeo yaliyotangazwa Novemba 19, mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Somaliland, Muse Yusuf Hassan, alisema kuwa idadi ya wapiga kura hao ilifikia asilimia 53.

Licha ya kuwa wapiga kura waliosajiliwa walikuwa ni milioni 1.2, ni 648,000 waliojitokeza kushiriki mchakato huo.

Uchaguzi kucheleweshwa

Uchaguzi wa Rais nchini Somaliland ulipangwa kufanyika mwaka 2022 lakini ulisogezwa mbele kutokana na sababu za kisiasa.

Shirika la Habari la Somalia (SONNA) lilisema kuwa uchaguzi huo ulikuwa wa amani.

TRT Afrika