Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu , ICC, ametoa wito wa kuwepo kwa njia mpya ya kukabiliana na uhalifu wa kivita katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
"Kumekuwa na kesi, kumekuwa na hatia nyingi , lakini kuna ukweli unaotutazama usoni... ubakaji haujakoma, uhalifu haujakoma," Karim Khan aliwaambia waandishi wa habari Jumatatu.
Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imekuwa ikikumbwa na makundi yenye silaha kwa miongo mitatu ambapo maelfu ya watu wameuawa na mamia ya maelfu wamehama makazi yao.
Mahakama ya ICC ilianzisha uchunguzi wake wa kwanza nchini DRC mwaka 2004, kufuatia rufaa ya serikali ya Kongo.
Hivi majuzi waziri wa sheria wa nchi hiyo aliiomba mahakama kuchunguza uhalifu unaodaiwa kufanywa na kundi la waasi la M23 katika jimbo la Kivu Kaskazini.
Khan yuko kwenye ziara ya kutafuta ukweli nchini ambapo alikutana na jamii zilizoathirika na walionusurika.
Pia alikutana na mshindi wa Tuzo ya Nobel Denis Mukwege - ambaye huwasaidia waathiriwa wa ubakaji.
"Tunamshukuru Karim Khan kwa ziara yake mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na tunatazamia ofisi yake kutanguliza uchunguzi na mashtaka yanayolenga kukomesha utamaduni wa kutokujali ambao umeenea kwa kiasi kikubwa," Mukwege alisema katika mtandao wake wa twitter.
Khan alihimiza kuwepo kwa "ushirikiano imara" kati ya serikali, magavana wa mikoa, mashirika ya kiraia, Umoja wa Afrika (AU), Umoja wa Ulaya (EU) na Umoja wa Mataifa (UN).
"Ujumbe ni tunahitaji kutafuta njia mpya ya kufanya kazi kwa maoni yangu, sio kwa njia sawa na ambayo tumekuwa tukifanya tangu 2004," mwendesha mashtaka alisema.