Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) inatarajia kusikiliza mashauri 19 yahusuyo nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kati ya Februari 17 na Machi 8, 2025, jijini Kigali nchini Rwanda.
EACJ, ambayo ina jukumu la kutafsiri sheria pamoja na kuzitekeleza kwa mujibu wa Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya EAC, itaketi nchini Rwanda kama utaratibu wa mzunguko wa mahakama hiyo.
Kati ya mwezi Februari na Machi, wafanyakazi wa Mahakama ya EACJ watahamia Kigali kutoka Arusha, Tanzania wakiwa na vitendea kazi vyao.
Hatua hiyo inalenga kuongeza uelewa wa ufanyaji kazi wa mahakama hiyo katika eneo la Afrika Mashariki, kulingana na Rais wa EACJ Nestor Kayobera.
“Tutasikiliza jumla ya mashauri 19 siku ya Februari 28,” alisema Jaji Kayobera siku ya Jumatatu.
Ikiwa nchini Rwanda, mahakama ya EACJ itaendesha mafunzo ya makosa ya kimtandao kwa majaji pamoja na kuwa na kikao kati ya majaji na mawakili, unaolenga kujadili masuala ya sheria ya biashara.
EACJ ilianzishwa mwaka 2001 ikiwa na jukumu la kuhakikisha kuwa sheria zote ndani ya nchi wanachama zinatafsiriwa kulingana na mkataba wa kuanzishwa kwa jumuiya hiyo.
Pia hutoa maoni na ushauri wa kisheria, pamoja na kujihusisha kwenye usuluhishi.