Juhudi za uokoaji zinaendelea baada ya mafuriko na maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha usiku kucha katika jimbo la Kivu Kusini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kuua zaidi ya watu kumi na mbili, afisa wa eneo hilo alisema.
Delphin Birimbi, kiongozi wa jamii ya Kalehe katika Kivu Kusini, alisema Ijumaa kuwa kulikuwa na watu 15 waliokufa katika kijiji chake na kwamba zaidi ya watu 30 hawajulikani walipo katika maeneo ya karibu ya Bushushu na Nyamukubi. Anahofia kuwa idadi ya vifo itaongezeka kwa kiasi kikubwa huku miili zaidi ikipatikana.
Mito miwili ilivunja kingo zake baada ya mvua kubwa iliyonyesha Alhamisi jioni na kumekuwa na maporomoko mengi ya ardhi huku nyumba nyingi zikiharibiwa, Birimbi alisema.
Waokoaji wanafanya kazi kutafuta na kuokoa mtu yeyote ambaye huenda amenaswa chini ya vifusi vya nyumba zao.
Katika taarifa iliyochapishwa Ijumaa, serikali ya mkoa wa Kivu Kusini ilitoa pole kwa familia zilizoathiriwa na kusema kuwa inatuma ujumbe kwenye eneo la tukio.
Mvua kubwa imeleta maafa kwa maelfu ya watu Afrika Mashariki, huku sehemu za Uganda na Kenya pia zikishuhudia mvua kubwa.
Mafuriko na maporomoko ya ardhi nchini Rwanda, ambayo inapakana na Kongo, yalisababisha vifo vya watu 129 mapema wiki hii.