Na Charles Mgbolu
Uzalendo, unaoelezewa kwa namna mbalimbali kuwa ni upendo usio na masharti, utii na nia ya kujitolea hata maisha ya mtu kwa ajili ya nchi, huwa na sura tofauti unapotazamwa kupitia maoni yanayotolewa na hali ya mazingira.
Uzalendo umebadilika na kuwa na uelewa wa kisasa zaidi na tafsiri ya kile ambacho raia wanahisi juu ya nchi, kutegemea na hali nzuri au mbaya ya nchi katika historia yake.
Kwa hivyo, uzalendo upo hali gani Nigeria huku kukiwa na maandamano dhidi ya mfumuko wa bei ambao umetoa matamshi tofauti ya hasira na hali ya kukata tamaa?
"Vijana wengi wa Nigeria wana hasira; wamekatishwa tamaa na hali ya sasa ya uchumi na kukosa kujisikia fahari kwa nchi," mwandishi wa habari Nnamdi Ojiego anaiambia TRT Afrika.
Dalili za wazi
Kutoka kwa waandamanaji kupeperusha bendera ya Urusi kwenye maandamano ya hivi majuzi katika baadhi ya maeneo ya nchi hadi kukataa kwa baadhi ya watu kuimba wimbo wa taifa, kuna hasira na kutoridhika kila mahali.
"Changamoto za kiuchumi nchini zinafanya mambo kuwa magumu sana. Wengi wanatafuta kila mbinu kudhihirisha kutoridhishwa kwao. Uzalendo, kama tunavyoujua, uko katika kiwango cha chini zaidi, haswa miongoni mwa vijana," anasema Ojiego.
Wakili anayeishi Lagos Ebuka Iwueze anaamini kuwa mapambano ya kiuchumi yamechangia hili, ingawa hapendi kile anachokiona kama vitendo visivyo vya kizalendo.
"Hali ya sasa ya uchumi sio sababu ya wewe kupeperusha bendera ya kigeni wakati wa maandamano. Kinyume chake, huwezi kumpiga mtoto kwa nguvu na kujizuia wakati mtoto analia," aeleza.
Kulingana na Iwueze, hasira inayochipuka nchini Nigeria kuhusu kupanda kwa gharama ya maisha tangu mwaka jana ilitarajiwa kuzuka wakati fulani.
"Wengine bila shaka wangeitikia hali hiyo kwa njia tofauti na wengine. Watu wamechanganyikiwa nchini Nigeria, ambako njaa na magonjwa yameenea. Kama watu wataona njia yoyote ya kutamka masikitiko yao, watatumia," anasema.
Hisia kali
Wengi wanaona kuongezeka kwa wimbi la chuki dhidi ya uzalendo, linalojidhihirisha katika vitendo vya uharibifu kando ya maandamano, kama ishara ya mambo yajayo na kutafuta hatua za haraka za kurekebisha.
Majaji wa Nigeria walizingatia kuweka kifungo cha miaka 10 jela kwa vitendo vinavyoonekana kuwa "vya uasi", kama vile "kuharibu alama za taifa" au "kukataa kukariri wimbo wa taifa na kuahidi utii".
Mswada uliopendekezwa ulipingwa baada ya kukosolewa vikali.
"Ilikuwa ni kosa, mbinu mbaya," anasema Iwueze juu ya hatua hiyo iliondolewa.
"Huwezi kutumia sheria kulazimisha watu kueleza hisia zao au kuonyesha vitendo vya uzalendo kwa uwazi."
Baadhi ya video zinazosambazwa mitandaoni za maandamano ya #EndBadGovernance zinaonyesha baadhi ya waandamanani wakipeperusha bendera ya Urusi na kuitaka Moskow "iwaokoe".
Hii hata ilisababisha ubalozi wa Urusi nchini Nigeria kufafanua kuwa hauhusiani na upeperushaji wa bendera.
Majibu ya sawa
Polisi wa Nigeria walisema zaidi ya watu 90 waliokuwa na bendera za Urusi walikamatwa.
“Itakuwa vigumu kuwatetea watu hawa mahakamani kwa sababu hali ya uchumi haiwezi kutumika kama kisingizio cha kufanya uhalifu,” anasema Iwueze.
Wanigeria wengi pia wanaamini kwamba mtazamo wa wanasiasa, ambao wanajitajirisha kwa fedha za umma na kuishi kwa kujionyesha, huongeza hasira na kusababisha raia kuwa na matumaini kidogo.
Ojiego anaamini kuwa kampeni za uhamasishaji wa kitaifa zinafaa kuanzishwa ili kuzuia vitendo kama hivyo.
"Tunaweza kuwadharau au kuwachukia wanasiasa, lakini lazima tufundishe watu kuipenda nchi yao na kufanya kila kitu ndani ya uwezo wetu kuilinda," anaiambia TRT Afrika.
Serikali ya Rais Bola Tinubu, kwa upande wake, imeomba raia kuwa na subira, ikiahidi sera zake zitazaa matunda hivi karibuni.
"Nimewaomba kwa uchungu sana wananchi wenzangu, tujitolee kidogo kwa ajili ya maisha ya nchi yetu. Kwa imani yenu kwetu, ninawahakikishia kuwa kujitolea kwenu haitakuwa bure," Tinubu alisema baada ya kuondoa ruzuku ya mafuta mwaka jana.
Wanigeria wanasema wamechoka kusubiri, lakini pengine hawana chaguo.
"Njia pekee ya kurejesha uzalendo wa papo hapo ni kufanya uchumi kufanya kazi tena. Wakati taifa linatoa njaa, kumshawishi mtu yeyote kuwa mzalendo ni vigumu," Iwueze anaiambia TRT Afrika.