Na
Abdulwasiu Hassan
Zaidi ya mwaka mmoja tangu serikali ya Rais Bola Tinubu kuchukua hatua na sera kali zaidi ya Nigeria katika historia ya hivi karibuni - kuondolewa kwa ruzuku ya mafuta - athari za kiuchumi, kijamii na kisiasa za hatua hiyo imewashangaza wengi.
Maamuzi ya Tinubu ya Mei 29, 2023 ya kuondoa ruzuku ya mafuta, imepandisha bei ya petroli kutoka karibu N190 (US$0.11) hadi N700 ($0.42) kwa lita, na kuathiri gharama ya maisha nchini kote.
Kubadili kiwango cha sarafu kwa wakati mmoja ili kuziba pengo kati ya viwango rasmi vya fedha na viwango vya soko kumesababisha sarafu ya Nigeria kushuka kutoka N470 hadi karibu N1,500 hadi dola moja.
Kwa hali ilivyo, taifa hilo la Afrika Magharibi linakabiliwa na gharama kubwa zaidi ya maisha kuwahi kutokea.
Mfumuko wa bei nchini Nigeria ulifikia asilimia 34.19 mwezi Juni, ikilinganishwa na asilimia 22.41 mwezi Mei 2023.
Raia wengi wa Nigeria wanaopanga kushiriki katika maandamano kutoka Agosti 1-10 juu ya kuongezeka kwa matatizo ya kiuchumi, wanahisi serikali inahitaji kubadili sera zake, ambazo wanaona kama chanzo kikuu cha tatizo.
Tishio la Maandamano
Hii si mara ya kwanza kwa Wanigeria kupinga waziwazi hatua za kubana matumizi zilizoanzishwa na serikali ilioko madarakani.
Mnamo Januari 2, 2012, umati wa raia waliingia barabarani kutoa maoni yao dhidi ya uamuzi wa serikali ya shirikisho wakati huo kuondoa ruzuku ya mafuta. Serikali ya Rais wa zamani Goodluck Jonathan ilieleza kuwa ruzuku ya mafuta ilihitajika kutolewa kwa sababu ilikuwa ya upotevu na haiwezi kudumu.
Hatua hiyo ilipandisha bei ya mafuta kutoka N65 hadi N141 usiku mmoja. Wanigeria walikataa.
Matokeo ya maandamano hayo, ambayo yalikuja kujulikana kama vuguvugu la "Occupy Nigeria", yalienea kutoka Abuja, Lagos, na baadhi ya miji mingine hadi sehemu kubwa ya nchi.
Baada ya siku nyingi za misukosuko, na kufa kwa baadhi ya watu huku wengi wakijeruhiwa, serikali ilibatilisha uamuzi wake. Zaidi ya miaka 12 baadaye, ruzuku ya mafuta imerudi kusumbua nchi na serikali ya sasa kwa njia zinazofanana.
Kutafuta Suluhu
Kadiri athari ya pamoja ya kuondolewa kwa ruzuku ya mafuta na kushuka kwa thamani ya naira inavyozidi kuumiza, serikali ya Rais Tinubu inaendelea kuweka sera za kupunguza athari za mabadiliko ya sera kwa wananchi wa kawaida.
Mojawapo ya hatua kama hizo ni kupandisha ajira ya kima cha chini cha mshahara kutoka N30,000 hadi N70,000 kupitia mswada ambao Rais ametia saini kuwa sheria.
Serikali haioni vizuri
Waandalizi wa maandamano hawakuweza kushawishika na juhudi za serikali za maridhiano na wito wa kusitisha maandamano kutoka pande tofauti tofauti.
"Serikali inahitaji macho mazuri. Wawakilishi wa serikali wa daraja ya chini lazima waangalie matamshi yao, tabia, na mwenendo kwa jumla. Wanahitaji kuwashawishi watu kuwa wako pamoja nao," Dk Abubakar Kari wa Chuo Kikuu cha Abuja aliiambia TRT Afrika.
Alisema ni vyema wajumbe wa bunge la Nigeria waachilie nusu ya mishahara yao kwa mshikamano na wananchi wanaoteseka kwa sababu ya kuongezeka kwa gharama ya maisha.
"Hiyo huenda ikawa sio nzuri ya kutosha, lakini kwa mwangalio ni mzuri kwa sasa," Dkt Kari alisema.
"Hata kama maandamano yaliyopangwa hayatafaulu wakati huu, yanaweza kuwa ya ghafla wakati ujao, katika hali ambayo haitakuwa rahisi kuishughulikia."
Ukweli kuhusu ruzuku ya mafuta
Wakati lita ya petroli inauzwa N700 kote Nigeria, gharama ya usafirishaji ni N1,117, kulingana na Major Energies Marketers Association of Nigeria.
Licha ya kuwa mzalishaji mkuu wa mafuta, Nigeria inategemea mafuta yaliyosafishwa kutoka nje kwa matumizi ya ndani. Kiwanda kipya cha kusafisha mafuta cha Dangote ni hatua nzuri ya kuiondoa nchi kutoka gharama ya usafirishaji, lakini hio haifanyiki kwa haraka.
NNPCL, mwagizaji pekee wa mafuta nchini, amekuwa akisema mara kwa mara nchi haiwezi kumudu kutoa ruzuku ya nishati.
Kwa kuzingatia mienendo ya uchumi, serikali inaweza kuvumilia kwa kiasi gani, na maandamano yataenedelea kuwa vipi?
Maafisa wakuu wa jeshi la polisi nchini Nigeria wameagizwa kuhakikisha kuwa raia wanaoshiriki maandamano yaliyopangwa hawapati madhara. Vikosi vya usalama vimewaonya waandamanaji dhidi ya matendo yoyote ya kuleta ghasia.
"Chochote kinaweza kutokea. Inaweza kuwa hasira tu isiyokuwa ya laizma. Inaweza kufurahiwa na kukubalika papo hapo," Dk Kari aliiambia TRT Afrika.
"Kumekua na maandamano Nigeria hapo awali, lakini kilicho tofauti wakati huu ni kiwango cha hasira na kutoridhishwa kwa wananchi kiko juu. Wanigeria wengi wanahisi hawana cha kupoteza."