Mahakama ya Libya imewafunga jela maafisa 12 kuhusiana na kuporomoka kwa mabwawa kadhaa huko Derna mwaka jana na kuua maelfu ya wakaazi wa mji huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisema Jumapili.
Maafisa hao waliokuwa na jukumu la kusimamia mabwawa ya nchi hiyo, walihukumiwa kifungo cha kati ya miaka 9 na 27 na Mahakama ya Rufaa huko Derna. Maafisa wanne waliachiliwa huru.
Derna, jiji la pwani lenye wakazi 125,000, liliharibiwa Septemba iliyopita na mafuriko makubwa yaliyosababishwa na Kimbunga Daniel.
Maelfu ya watu waliuawa na maelfu wengine hawajulikani waliko kutokana na mafuriko hayo yaliyopasua mabwawa, kusomba majengo na kuharibu vitongoji vyote.
Mwanasheria Mkuu wa Tripoli alisema washtakiwa watatu waliamriwa "kurejesha pesa zilizopatikana kutokana na faida haramu", kulingana na taarifa, ambayo haikutoa majina au nafasi za wale walio kwenye kesi.
"Maafisa waliopatikana na hatia wameshtakiwa kwa uzembe, mauaji ya kukusudia na ufujaji wa pesa za umma," chanzo cha mahakama huko Derna kiliiambia Reuters kwa njia ya simu, na kuongeza kuwa walikuwa na haki ya kukata rufaa dhidi ya hukumu hizo.
Ripoti ya mwezi Januari ya Benki ya Dunia, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya ilisema mafuriko makubwa ya ghafla huko Derna yalisababisha janga la hali ya hewa na mazingira ambalo lilihitaji dola bilioni 1.8 kufadhili ujenzi na ukarabati.
Ripoti hiyo ilisema kubomoka kwa mabwawa hayo kwa kiasi fulani kunatokana na muundo wake, kulingana na taarifa za kihaidrolojia zilizopitwa na wakati, na kwa sehemu ni matokeo ya matengenezo duni na matatizo ya utawala wakati wa zaidi ya muongo mmoja wa vita nchini Libya.