Na Brian Okoth
Ukraine ni mojawapo ya wauzaji wakubwa wa nafaka duniani, kwa kawaida husambaza karibu tani milioni 45 za nafaka kwenye soko la kimataifa kila mwaka.
Walakini, baada ya Urusi kuanzisha vita dhidi ya nchi hiyo mnamo Februari 2022, tani za nafaka zilirundikana kwenye maghala huku meli zikishindwa kupata njia salama kutoka bandari za Ukraine.
Matokeo yake yalikuwa ni ongezeko kubwa la bei za vyakula vikuu kote ulimwenguni. Bei za nishati pia zilikuwa juu mnamo 2022, na kulazimisha mataifa yanayoendelea kubeba mzigo mkubwa.
Usafirishaji wa Chakula licha ya vita
Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi ulifikiwa 18 Juali 2022, baada ya upatanishi wa Uturuki na Umoja wa mataifa.
Mpango huo umefanywa upya mara kwa mara na Urusi na Ukraine ikiwa awamu ya hivi majuzi ambayo ilidumu kwa siku 60 imekwisha Juali 17.
Mpango huo, umeshuhudia takriban mabara yote yakipokea nafaka kutoka Ukraine lich ya vita.
Angalau tani milioni 32.8 za nafaka, ikiwa ni pamoja na ngano, mahindi, shayiri, alizeti na maharagwe ya soya, zimesafirishwa kutoka Ukraine hadi sasa, kulingana na Umoja wa Mataifa (UN).
Zaidi ya meli 1,000 zimesafirisha vyakula hadi sehemu tofauti duniani.
Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa Afrika inachukua asilimia 12.26 ya nafaka inayoagizwa kutoka Ukraine, wakati mataifa mengine duniani, ikiwa ni pamoja na Asia na Ulaya, yanachukua 87.74% ya jumla ya usafirishaji wa nafaka.
Afrika imenufaika
Shashwat Saraf, Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Mashariki wa Kamati ya Kimataifa ya Uokoaji, anasema kushindwa kurejesha mpango wa nafaka kunaweza kusababisha "kuyumba kwa soko la chakula duniani."
“Nchi za Afrika Mashariki na sehemu nyingine za dunia zinategemea uagizaji wa chakula ili kupunguza uhaba katika soko la ndani. Ikiwa kuendelezwa kwa mpango wa nafaka hautawezekana, uhaba wa chakula katika mataifa yanayoendelea utazidi kuwa mbaya zaidi," Saraf anaiambia TRT Afrika.
Abdikadir Bille, mkulima na mhusika mkuu katika sekta ya kilimo nchini Somalia, pia anasema kurefushwa kwa mpango wa nafaka kutanufaisha sana Afrika.
“Kutokana na ukame wa muda mrefu katika eneo la Pembe ya Afŕika, mamilioni ya watu wamekabiliwa na mgogoŕo wa njaa. Nina matumaini pande husika zitaongeza mpango wa nafaka ili kuepusha utapiamlo na vifo vinavyosababishwa na njaa,” anaiambia TRT Afrika.
Kuangazia Afrika
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alisema kuongezwa kwa muda wa mpango huo baad ya tarehe 17 Julai ni muhimu kwa ajili ya Afrika na mataifa mengine yanayoendelea, ambayo usalama wao wa chakula unategemea kwa kiasi kikubwa nafaka ya Ukraine.
Rais Erdogan alipendekeza mpango huo uongezwe kwa miezi mitatu mingine, badala ya miwili, ili kuzinufaisha nchi za Kiafrika ambazo zinahitaji sana usafirishaji wa nafaka kutoka Ukraine.
Iwapo mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi utaporomoka, "utaiathiri Afrika Mashariki kwa nguvu sana," Dominique Ferretti, afisa mkuu wa dharura wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani katika eneo hilo, alisema mwishoni mwa Juni.
Hadi kufikia Agosti 2022, takriban watu zaidi ya milioni 139 katika nchi 35 za Afrika walikuwa wakikabiliwa na janga la njaa au hali mbaya zaidi ya uhaba wa chakula. UN inakadiria kuwa idadi ya waathiriwa wa njaa inaweza kuwa kubwa zaidi.
Mpango wa mauzo ya nje "ni muhimu kabisa, sio tu kwa Afrika Mashariki bali kote Afrika," Ferretti alisema katika mji mkuu wa Kenya Nairobi wakati wa mahojiano na vyombo vya habari.
Hali ya hatari
Njaa imesababisha kutangazwa kwa hali ya hatari katika baadhi ya nchi, ikiwa ni pamoja na Kenya hapo awali, na Nigeria kwa sasa. Wanufaika wakuu wa Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi barani Afrika ni Misri, Tunisia, Kenya, Ethiopia, Algeria, Sudan, Libya na Somalia, kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa.
Nchi nyingi za kipato cha chini barani Afrika huagiza mafuta ya alizeti na ngano kutoka Ukraine, wakati nchi kadhaa za kipato cha chini husafirisha mafuta ya soya, mahindi, mafuta ya alizeti, shayiri na ngano kutoka Ukraine.
Misri, inayoongoza barani humo katika uagizaji wa nafaka, inaleta ngano, mahindi na maharagwe ya soya kutoka Ukraine, huku Kenya ikisafirisha ngano na mahindi.
Ngano na mafuta ya alizeti hufanyiza shehena kubwa zaidi ya nafaka hadi Ethiopia, huku Algeria ikisafirisha sehemu kubwa ya ngano na shayiri kutoka Ukrainia.
Chini ya Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) shehena za kibinadamu, Ethiopia imenufaika zaidi, huku tani 263,000 za metriki (36%) zikisafirishwa hadi nchini humo.
Sudan inafuatia kwa tani 30,000 (4%) na kisha Kenya na Somalia zenye tani 25,000 kila moja (3%). Djibouti ni taifa jingine ambalo limefaidika na mauzo ya nje ya WFP, likiwa na tani 1,000 za metriki.