Ripoti ya shirika la kimataifa la uhamiaji ,IOM inaonyesha kuwa uhamiaji wa watu kutoka Ethiopia, Somalia, na Djibouti kupitia Yemen, katika njia inayojulikana kama njia ya Mashariki ya Uhamiaji, umeongezeka kwa 64% mnamo 2021.
Wakati wengine wanahama kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi, wengine wanahepa migogoro, na wengine kushawishiwa na wasafirishaji haramu wa binadamu ambao huwaambia watapata kazi nzuri kwenye ghuba.
Hata hivi ripoti mpya ya IOM ambayo imezinduliwa, inayoangazia mwaka 2022, inasema kuwa kuna uhamiaji mkubwa ndani ya nchi za Afrika mashariki na Pembe ya Afrika ambao una thamani.
Je , ripoti hii imeonyesha nini?
Ripoti hii mpya inasema kuwa kanda ya mashariki na Pembe ya Afrika ina takriban watu nusu bilioni. Kati ya hawa takriban milioni 8.5 walirekodiwa kama wahamiaji mwaka 2021.
Ingawa idadi hii ya wahamiaji inawakilisha chini ya asilimia mbili ya watu wote, mwelekeo unaonyesha kuwa uhamiaji wa wananchi wa kanda hii unaongezeka .
Watafiti wanasema kuwa ikisimamiwa vizuri uhamiaji wa watu una uwezo wa kuchangia maendeleo ya mataifa na kuinua kaya nyingi kutoka kwenye umaskini.
“ Kenya, Rwanda, na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni miongoni mwa nchi nane za Afrika ambazo zimejiunga na mpango wa biashara elekezi chini ya mfumo wa kibara wa biashara yaani AfCFTA . Hii inaashiria kuanza rasmi kwa biashara halisi chini ya sheria za AfCFTA,” ripoti inasema .
Hata hivyo wanasisitiza kuwa ili uhamiaji unufaishe biashara ni lazima uhuru wa kuvuka mipaka kwa ajili ya wafanyikazi urahisishwe.
“Mnamo Julai 2022, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuwa mwanachama wa saba wa jumuiya ya Afrika mashariki, ilitoa nafasi ya kufanya eneo hili kuwa mojawapo ya jumuiya za kiuchumi za kikanda zilizopanuka zaidi na takriban watu milioni 300, wanaowakilisha robo ya wakaazi wa Afrika”.
Hata hivyo ripoti hiyo inakashifu sera ngumu za biashara ndani ya eneo la Afrika mashariki na pembe ya Afrika kama ushirikiano mdogo wa mipaka kati ya nchi husika.
Nchi mbalimbali za Afrika bado zinaendelea kupambana na matukio ya uhamiaji haramu unaofanyika kwenda ndani au nchi ya bara hilo.