Ripoti mpya iliyotolewa na UNAIDS inaonyesha kuwa watu milioni 39 duniani kote walikuwa wanaishi na ukimwi / Picha: AP

Shirika la Umoja wa mataifa linaloangazia Ukimwi limetoa wito kwa uongozi thabiti wa kisiasa ili kumaliza maambukizi ya ukimwi.

"Maambuki ya Ukimwi yanaweza kufanikiwa yanapojikita katika uongozi wa kisiasa, na yanaimarishwa wakati jumuiya zinaruhusiwa kutekeleza jukumu lao,"amesema mkurugenzi mkuu wa UNAIDS Winnie Byanyima.

Dkt, Byanyima ameongea katika uvumbuzi wa ripoti ya 2023 inayoangazia hali ya maambukizi ya ukimwi duniani.

UNAIDS imevumbua ripoti mpya inayoitwa " Njia Inayokomesha ukimwi"

"Njia inayomaliza ukimwi sio siri, ni chaguo la kisiasa na kifedha," Byanyima ameongezea.

Data za 2022 kwa mujibu wa ripoti hiyo

  • Watu milioni 39 duniani kote walikuwa wanaishi na virusi vya UKIMWI
  • Watu milioni 29.8 walikuwa wakipokea dawa za ARV
  • Watu milioni 1.3 waliambukizwa virusi vya UKIMWI
  • Watu 630,000 walikufa kutokana na magonjwa yanayohusiana na UKIMWI

Ripoti hiyo inaonyesha pia kuwa, Botswana, Eswatini, Rwanda, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Zimbabwe tayari zimefikia malengo ya "95-95-95".

Hiyo ina maana 95% ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi wakijua hali yao , 95% ya watu wanaojua kuwa wanaishi na ukimwi wanatumia dawa za kuokoa maisha, na 95% ya watu wanaopata matibabu wamekandamiza virusi.

Ripoti hiyo inaangazia kwamba kupunguza maambukizi ya ukimwi hufaulu wakati nchi imejikita katika uongozi thabiti wa kisiasa.

Hii inamaanisha kufuata data, sayansi, na ushahidi; kukabiliana na ukosefu wa usawa unaorudisha nyuma maendeleo; kuwezesha jumuiya na asasi za kiraia katika jukumu lao muhimu katika mwitikio; na kuhakikisha ufadhili wa kutosha na endelevu.

UNAIDS inasema maendeleo ya kupambana na ugonjwa huu yamekuwa makubwa katika nchi na kanda ambazo zina uwekezaji mkubwa zaidi wa kifedha, kama vile Mashariki na Kusini mwa Afrika ambapo maambukizi mapya ya UKIMWI yamepungua kwa 57% tangu 2010.

Idadi ya watu wanaopata matibabu ya kupunguza makali ya ukimwi imeongezeka kutoka milioni 7.7 mwaka 2010 hadi milioni 29.8 mwaka 2022.

Hata hivyo, ripoti hiyo pia inaeleza kuwa kukomesha UKIMWI hakutakuja moja kwa moja.

Takriban watu milioni 9.2 bado wanakosa matibabu, wakiwemo watoto 660,000 wanaoishi na ukimwi.

TRT Afrika